• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
Kibagare Slums yajiweka pazuri kuwania ubabe wa Nairobi Magharibi

Kibagare Slums yajiweka pazuri kuwania ubabe wa Nairobi Magharibi

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kibagare Slums ni kati ya vikosi ambavyo vimeonyesha bayana kuwa vimepania kupambana mwanzo mwisho kwenye mechi za kuwania Ligi ya Kaunti ya Nairobi Magharibi muhula huu.

Kibagare Slums ya kocha, Johnstone Etale ni miongoni mwa timu 22 zinazoshiriki kampeni za Kundi C kupigania tiketi ya kushiriki kipute cha Nairobi West Regional League (NWRL) msimu ujao.

Klabu hii ambayo hupatikana katika mtaa wa Kibagare iliasisiwa miaka 15 iliyopita kwa lengo la kukuza talanta za wanasoka chipukizi kutoka eneo hilo.

Afisa mkuu wake, Joseph Itotia alisema: ”Ingawa tumekaa vizuri kufanya kweli kwenye kampeni za msimu huu, tatizo ni kuwa janga la virusi vya corona linazidi kuzoa mazito kwani limechangia shughuli za michezo kupigwa breki tena.”

Afisa huyo anasema licha ya shughuli za michezo kusitishwa bado wanalenga kumaliza kati ya nafasi mbili bora ili kujiweka pazuri kupandishwa ngazi.

Katika msimamo wa mechi za ngarambe ya msimu huu baada ya kucheza mechi tatu, Kibagare Slums inashikilia nafasi ya sita kwa alama sita, sawa na Lockdown FC, Red Cross FC, Gachui Black Boots FC na LSA FC tofauti ikiwa idadi ya mabao. Nayo Maroon Young Stars FC imetua kileleni kwa kuzoa 11, moja mbele ya Kasikasi FC na Dumberi Allstars FC tofauti ikiwa idadi magoli.

Tiketi ya kusonga mbele

Meneja huyo anasema kuwa wameshiriki ligi ya kaunti kwa misimu mitano ambapo raundi hii hawana la ziada bali itawabidi wapambane kiume ili kutimiza azimio hilo.

Ndani ya kipindi hicho Kibagare Slums inajivunia kuibuka nambari mbili kwenye mechi za ngarambe ya mwaka 2014.

”Licha ya changamoto za uhaba wa ufadhili tunaamini tuna wachezaji wazuri ambapo tukibahatika kupata sapoti ndani ya mihula miwili tu bila kujipigia debe tutafanya kinyume na matarajio ya wengi na kupanda ngazi,” anasema.

Naibu wake ni Simon Kimeu. Hata hivyo anatoa wito kwa viongozi wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) wazamie mpango wa kutafuta wafadhili kusaidia timu za mashinani kunoa makucha ya wachezaji chipukizi.

Betika National Super League (BNSL)

Katika mpango mzima meneja wake, Christopher Njenga anasema ndani ya miaka mitano ijayo wanadhamiria kuwa wakicheza mechi za Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL) kupigania kufuzu kwa Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Ukosefu wa ufadhili kwa muda umefanya Kibagare ishindwe kugharamia mahitaji ya kuendesha shughuli zao michezoni. Kibagare ambayo mechi za ligi huchezea Uwanjani Kihumbu-ini Kangemi tangia ibuniwe mwaka 2015 inajivunia kulea wachezaji kadhaa waliokwenda kwingine akiwamo Amstone Agama (Gogo Boys).

You can share this post!

Kimbunga Jobo chaishiwa nguvu baada ya kuwasili Tanzania

TAHARIRI: Serikali iharakishe kandarasi mpya