• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
TALANTA YANGU: Kijana mkwasi wa vipaji atia fora

TALANTA YANGU: Kijana mkwasi wa vipaji atia fora

NA PATRICK KILAVUKA

MSUKUMO, ari, bidii ya mchwa, nidhamu na pia mawasilisho ya gazeti ya Taifa Leo na mitihani iliyochapishwa gazetini, ushirikiano mwema na wazazi, walimu na wanafunzi ni mambo yaliyochangia kufaulu kwake katika masomo

Mwanafunzi Craig Njeka Ndede, 15, wa Shule ya msingi ya Visa Oshwal, Westlands, Nairobi alikuwa simba wa shule hiyo kwa kupata alama 414.

Mbali na kuwa mwanafunzi mpevu katika masuala ya Sayansi ambapo alitunukiwa tuzo wakati wa mashindano ya masuala ya Sayansi baina ya wanafunzi wa shule mbalimbali baada ya kuibuka mweledi katika kujibu masuala ya kisayansi awali.

Isitoshe, husakata kabumbu kama njia ya kukuza talanta zake za masomo na vipawa ambapo alicheza kama kiungo shuleni na timu ya RIAT, Homa Bay.

Craig ni mwana pili katika familia ya watoto watatu wa Bw Joseph Ndede na Bi. Lydia Ndede.

Anasema alikuwa anaanza pilkapilka za masomo kuanzia saa 4.40 asubuhi hadi saa 10.30 usiku akiyapa masomo yenye kizungumti kwake kipaumbele kusawazisha alama zake na alivuna matunda ya jasho lake katika masomo ya Hisabati, Sayansi, Kiswahili na Kiingereza.

Pia, alitumia mbinu ya kuuliza walimu maswali kwa wingi, mijadala ya vikundi na kutia bidii kama njia ya uwianisho wa masuala yake ya kiakademia pamoja na kuweka imani yake kwa Mola majalia yote.

Mchango wa walimu

Anautaja mchango wa walimu pamoja na kuwa na imani naye, ujasiri, chakula chenye lishe bora shuleni na nyumbani, mazingira faafu ya masomo shuleni na nyumbani kuwa pia changizo za alama yake bora. Fauka na kutokuwa na msongo wa mawazo kutatiza masomo yake kwa miaka minane amesoma.

Mwalimu wa Lugha wa shuleni na mkurungenzi wa shule walikuwa na furaha riboribo wakimtaja kama simba wa shule hiyo.

Mwalimu Jonadab Ondara alisema kwamba Craig alionyesha kwamba ana uwezo wa kufanya vyema kutokana na bidii kwani alikuwa msomi wa vitabu vya waandishi waliobobea. Mbali na kushiriki katika uandishi wa mitungo kila Ijumaa na mijadala.

Pia, alizoea kufanya mazoezi ya ziada hali ambayo iliimarisha matokeo yake kwani alikuwa chini sana katika somo hilo. Hata hivyo, alisawazisha na kuibuka miongoni mwa wanafunzi 58 ambao walipata A- hadi A shuleni katika Kiswahili.

Mzazi wake Bw Ndede alimsawiri kama mtoto aliyekuwa na msukumo wa kipekee katika familia na hakuwa anashinikizwa kusoma bali alikuwa na ari ya kutaka kujua na angeamka mapema na kulala akiwa amechelewa.

Alikuwa hata anasoma na wanafunzi wa kidato cha tatu na nne shuleni anakofunza.

 

Craig Njeka Ndede (wa pili kulia) akifurahia ushindi wake akiwa na mzazi wake Joseph Ndede (kushoto) pamoja na walimu wa Shule ya Msingi ya Visa Oshwal, Westlands, Nairobi. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Craig angependa kujiunga na Shule ya Wavulana ya Alliance anakootea kujijengea msingi wa ushindani ambao utamwezesha kujizoelea alama bora za kusomea digrii katika fani ya dawa akilenga kuwa chambo cha kuimarisha afya ya wananchi wanaohangaishwa na magonjwa akikumbuka yale Mualana amemtendea kwa kupita mtihani.

Uraibu wake ni kusoma vitabu vya hadhithi akiwa anavutiwa na mwandishi Dickens.

Angependa kushukuru Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake, wazazi, walimu, wanafunzi wenza na majirani kwa msaada wao na himizo kwa njia moja au nyingine pamoja na kufurahi kwa udhati ufanisi wake.

Pili, anamhongera mwalimu wa darasa na mlezi wake wa Kiswahili na Hisabati Philis Kamau pamoja na mwalimu wa Idara ya Kiswahili Bw Ondara kwa makuzi.

Ushauri wake kwa wanafunzi walio nyuma yake ni kwamba, licha ya mabonde na milima masomoni, kuna siku njema na wanafaa kuwa wastahamilivu, watie bidii, wenye kujiamini wanaweza na kubwa zaidi- wamtumaini na kumuamini Mungu.

You can share this post!

WANTO WARUI: Serikali itafute chanzo cha matokeo duni...

Tottenham watandika Newcastle United na kuingia nne-bora EPL

T L