• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
TALANTA YANGU: Mwanaskauti wa kuigwa

TALANTA YANGU: Mwanaskauti wa kuigwa

Na PATRICK KILAVUKA

ANASEMA mshawasha wake wa kuwa kiongozi unatokana na vile kiongozi wa upinzani Raila Amollo Odinga hujisuka kisiasa na kuwa kiongozi mtajika na anayependwa na hadhira.

Isitoshe, ukakamavu na ujasiri wa Raila na utu alionao katika kuteleza majukumu yake wakati anawatetea raia, unamtia motisha zaidi.

Marine Adema,15, ni naibu kamanda wa maskauti na kiranja wa darasa la nane katika shule ya msingi ya Kihumbuini, Kangemi, kaunti ndogo ya Westlands, Kaunti ya Nairobi.

Yeye ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto watano wa Bw Antony Mugita Salamba na Bi Rose Nyangai Shikami.

Anasema ni kutokana na sera zake murua ambapo wanaskauti na wanafunzi wa darasa lake walimchagua kuwa kiongozi wao.

Wakati wa kampeni zake kama mwanaskauti, aliwarai wenzake kumpigia kura kwa sababu aliamini anaweza kuonyesha ushujaa wakati anapotekeleza majukumu, kuimarisha nidhamu, kusaidia wengine katika jamii na kikundi, pamoja na kuwaahidi kuenda kwenye seminaa kama njia ya kujifunza mengi kuhusu mitindo ya maisha, maadili mema na uimarishaji wa uraia au uzalendo. Aliteka hisia za wanaskauti wengine na kuibuka mshindi kwa kura 15 dhidi ya moja ya mpinzani wake.

Kama ishara ya kuongoza kwa vitendo, alihimiza wenzake kusaidia familia ya mmoja wao kwa kuwapa chakula, mafuta ya kupika na sabuni.

Katika kukuza maskauti wengine, amekuwa kielelezo cha Acilian Khageha, Timothy Kipsoi na Catherine Vuyanzi ambao wanapitia katika mkondo wake kujiimarisha kuwa maskauti.

Ubora wake katika uongozi unatokana na moyo wa utu alioukuza baina ya wanafunzi na mtagagusano wa kirafiki alionao kwao. Mbali na wakati ambapo wanapata changamoto ambayo anaweza kuishughulikia, ile ambayo inahitaji busara zaidi, yeye huipeleka kwa mwalimu au mkuu kama njia ya kutafuta suluhisho la kudumu.

You can share this post!

Kocha Vihiga Queens asema hakuna kulaza damu Ligi Kuu

Simiu na Jeruto moto wa kuotea mbali mbio za nyika za...

T L