• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
ODONGO: Tishio kwa handisheki ni tishio kwa amani nchini

ODONGO: Tishio kwa handisheki ni tishio kwa amani nchini

Na CECIL ODONGO

HUKU taifa likiadhimisha miaka mitatu ya ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa upinzani Raila Odinga, muafaka kati ya wawili hao sasa upo hatarini kuvurugika kutokana na siasa za uchaguzi wa 2022.

Wandani wa Bw Odinga wakiongozwa na Seneta wa Siaya James Orengo na mbunge wa Rarieda Otiende Amollo wanadai kuwa kuna njama inayosukwa na baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa serikalini kufifisha umaarufu wa Bw Odinga.

Wanasiasa wao wamelalamika kwamba Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Karanja Kibicho ndiye anatumiwa kusuka njama hizo ili kumlemaza kabisa Bw Odinga kisiasa.

Matukio hayo yanajiri wakati ambapo muafaka huo upo katika hatua muhimu kwa kuwa mabunge ya kaunti yameshapitisha ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) ambayo ikiidhinishwa na bunge, basi raia wataelekea kwenye kura ya maamuzi kufikia Juni.

Hata hivyo, misukosuko hii ilitarajiwa kwa kuwa hakuna hasa anayefahamu kwa undani yaliyoafikiwa kati ya Rais na Bw Odinga walipozika tofauti zao na kuamua kufanya kazi pamoja.

Ingawa wawili hao wamekuwa wakisisitiza kuwa makubaliano kati yao hayakuhusu 2022 kwa nini viongozi na wafuasi wa Bw Odinga huingiwa na wasiwasi kuhusu kukosa uungwaji mkono wa Rais ?

Ni bayana kwamba uhusiano wa Bw Odinga na waliokuwa vinara wenza katika muungano wa Nasa ulivurugwa baada ya kuanzisha uhusiano kati yake na Rais Kenyatta bila kuwahusisha.

Iwapo ushirikiano wake na Rais utavurugika atakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha anapata uungwaji mkono aliokuwa nao katika uchaguzi wa 2017 ambao alidai alipokonywa ushindi.

Kwa upande mwingine kama itatokea kuwa Bw Odinga atasalitiwa kuhusu ‘handisheki’ basi Rais atakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha kuwa mwaniaji ambaye atamuunga mkono ana umaarufu miongoni mwa wapiga kura.

Aidha hata akisalitiwa itakuwa ngumu sana kummaliza Bw Odinga kisiasa kwa kuwa wengi walitabiri mwisho wake hata baada ya chaguzi zilizopita lakini akajiinua na kurejelea umaarufu wake wa awali.

Wengi walitabiri kwamba Bw Odinga angeisha kisiasa katika chaguzi za 2013 na 2017 lakini waziri huyo mkuu wa zamani alivumbua mbinu kadhaa ya kudumisha umaarufu wake kisiasa. Kwa hivyo, hoja kwamba kutamatika kwa ‘handisheki’ itakuwa mwisho wake kisiasa haina mashiko.

Kumsaliti kupitia handisheki kutawapa wafuasi wake ari ya mpya ya kurejelea uanaharakati wao kama miaka ya nyuma huku wakitumia hali ngumu ya kiuchumi kukosoa serikali.

Hata hivyo, ni wazi kwamba siasa za 2022 zimekaribia wala hawezi kuzungumzia ‘handisheki’ bila kuihusisha na nafasi ya urais wa 2022. Iwapo ni kweli kwamba kuna njama ya kumsaliti Bw Odinga na Dkt Ruto, basi pia itakuwa vigumu kwa Rais kuwaelezea Wakenya kwa nini aliamua kufanya kazi nao.

Ushirikiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga umehakikisha taifa lina amani na unafaa kuendelea ili miradi iliyoanzisha ikalimilike na mabadiliko ya katiba pia yatimie.

You can share this post!

TAHARIRI: Matatizo ya CBC yatatuliwe upesi

WANGARI: Duale amegonga ndipo kuhusu video za ngono