• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
WANGARI: Duale amegonga ndipo kuhusu video za ngono

WANGARI: Duale amegonga ndipo kuhusu video za ngono

Na MARY WANGARI

MBUNGE wa Garissa Aden Duale, aliibua hisia kali majuzi kuhusiana na mswada aliopendekeza kwa lengo la kupiga marufuku usambazaji wa matini za ngono mitandaoni.

Kwa kufanyia marekebisho Kifungu cha Sheria kuhusu Matumizi Mabaya ya Tarakilishi na Hatia Mitandaoni, 2018, Duale, aliyewahi kuhudumu kama kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa, alikusudia kufanya uchapishaji wa video za ngono katika mitandao ya kijamii kuwa hatia.

Baadhi ya wengi walikerwa na hatua hiyo na kufurika mitandaoni kuelezea hisia zao.

Kunao waliohoji kuwa kutazama au kutotazama video za ngono ni uamuzi wa mtu binafsi na zaidi kufanya hivyo hakusababishi tishio lolote dhidi ya usalama wa taifa.

Wengine walihisi kuwa kuna masuala chungunzima yenye uzito yanayopaswa kuangaziwa kama vile mikakati ya kusambaza chanjo ya Covid-19 nchini, ufisadi, mashambulizi ya kigaidi na kadhalika.

Ingawa hoja hizo zina msingi kwa kiasi fulani, hatuwezi kupuuza athari ya matini za ngono zilizofurika mitandaoni dhidi ya mtu binafsi na jamii nchini Kenya kwa jumla.

Katika miaka ya hivi majuzi, hasa kutokana na maendeleo ya kidijitali na kiutandawazi, video na matini nyinginezo za ngono zimefurika mno mitandaoni.

Kutokona na upatikanaji kirahisi wa vifaa vya kielektroniki kama vile simu za kisasa, tarakilishi na vipakatalishi, anachohitaji mtazamaji ni kubonyeza tu na kuanza kujifurahisha pasipo kujali umri, hadhi au jinsia yake.

Uhalisia ambao huwezi kupuuzwa ni kuwa, utazamaji wa video hizo za ngono una athari ya moja kwa moja dhidi ya mtazamaji iwe ni kimawazo au hata kisaikolojia.

Ndiposa suala hilo linalohusu maadili ya umma, linahitaji kuangaziwa kwa dharura kwa maslahi ya jamii nchini.

Tafiti tayari zimeashiria uzito wa jambo hilo huku ripoti mpya ikiorodhesha Kenya miongoni mwa mataifa yenye watazamaji wengi zaidi wa matini za ngono Barani Afrika, pamoja na Afrika Kusini na Nigeria.

Wataalam wa sosholojia wamethibitisha kuwa matini za ngono zinazidisha ukosefu wa usawa kijinsia kwa kuwasawiri isivyofaa wanawake na wanaume.

Kando na kusambaza kasumba potovu kuhusu tendo la ndoa, matini hizo huwaashiria wanaume kama viumbe katili wanaopata raha kwa kuwadhalilisha wanawake, huku wanawake nao wakisaswiriwa kama viumbe dhaifu wanaopenda kudhulumiwa na kudunishwa.

Kwa kujaribu kuiga wanachotazama kwenye video hizo, si ajabu kuwa wanaume wengi hugeuka katili na matokeo yake ni kuongezeka kwa visa kama vile unajisi, ubakaji na dhuluma za kinyumbani.

Huku serikali ikijitahidi kufanikisha usawa wa kijinsia kuambatana na viwango vya kimataifa, ni sharti wadau husika waingilie kati kwa kubuni sera na sheria kabambe ili kudhibiti usambazaji wa matini za ngono mitandaoni.

[email protected]

You can share this post!

ODONGO: Tishio kwa handisheki ni tishio kwa amani nchini

SHINA LA UHAI: Ng’amua ukweli kuhusu chanjo ya corona