• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:16 PM
UFUGAJI: Ulemavu kwake si kikwazo, umempa nguvu ya kujituma

UFUGAJI: Ulemavu kwake si kikwazo, umempa nguvu ya kujituma

NA LABAAN SHABAAN

FRANCIS Muiruri alilemaa kwa sababu ya ugonjwa wa polio akiwa mchanga.

Sasa ni mume na baba wa mtoto mmoja na ulemavu wa mguu haujamzuia kufanya kazi mseto kujitegea uchumi ili kujitegemea.

Akilimali ilipomtembelea Witeithie, eneobunge la Juja, Kaunti ya Kiambu, tulimkuta akinyunyizia maji vijishamba vinavyoning’inia kutani nyumbani mwake anakofugia kuku vizimbani.

Bw Francis Muiruri anyunyizia maji vijishamba vya mboga nyumbani kwake Witeithie, Kaunti ya Kiambu. PICHA | LABAAN SHABAAN

Licha ya hali yake inayomlazimu kutumia magongo kupata mwendo, Muiruri anajikaza kisabuni kufanikisha kilimo na ufugaji kuongeza mapato kwa anayopata kutoka kwa kazi ya uhasibu katika Serikali ya Kaunti ya Kiambu.

“Inanibidi kuratibu muda wangu vyema ili nifanye kazi hizi zote. Aghalabu mimi hufundisha watu kuhusu utumizi wa vizimba katika ufugaji kuku kila mwisho wa juma ama baada ya kazi,” Muiruri anasema.

Katika thumni ya ekari ya shamba ambamo amejenga maskani yake, Muiruri ametenga sehemu kufugia kuku zaidi ya 100 huku sehemu nyingine zikiwa na mbwa, ndege na vibanda alivyotumia kufugia nguruwe awali.

“Sana sana watu wananijua kwa utaalamu wa kufuga kuku vizimbani. Ndio mtindo wa kisasa ambao unarahisisha na kuzidisha mapato ya wafugaji kuku katika sehemu finyu,” anaeleza.

“Wafugaji kuku wanaotumia mitindo wazi wana changamoto nyingi kama vile hatari ya maambukizi ya magonjwa, utumizi sehemu kubwa, kuku kushambuliwa na wanyama na mapato madogo yanayokuja kwa kufanya kazi nyingi,” Muiruri anaongeza.

Kwa mujibu wa mhasibu huyu, yeye hukumbatia sheria inayowaepusha wanaoishi na ulemavu kulipa ushuru ili kuimarisha biashara yake ya kukita vizimba sehemu tofauti nchini.

Muiruri huagiza vizimba kutoka China bila kulipa kodi.

Kupitia mitandao ya kijamii yeye hujipigia debe ili avune wateja. Wengi wa wateja wake humfikia kupitia mtandao wa Facebook ambapo ana wafuasi wa kupigiwa mfano.

Mkulima na mfugaji huyu anasema alianza biashara hii mwaka wa 2019 na kufikia sasa amekita vizimba 15 kwa wafugaji kuku.

Gharama ya kukita vizimba kikamilifu kwa mkulima mmoja ni Sh140,000. Mpango huu unahusisha muundo unaobeba ndege 128. Kwa gharama hii mfugaji anauziwa pia kuku walio tayari kutaga.

“Ukilipa Sh140, 000 pia tutakupa chakula cha kuku kilo 70 kuwalisha kwa wiki moja. Baada ya siku chache utaanza kupata mayai na tutakupa hata soko la mayai,” Muiruri anadokeza.

Jina la Shamba lake ni Maono Farm. Ni shamba toshelevu kwake kukidhi mahitaji yake licha ya kuwa ameajiriwa na Kaunti ya Kiambu.

Kutoka hapa, Muiruri hupata maziwa ya mbuzi, mboga, mayai, nyama na ulinzi kwani anafuga mbwa.

“Nina mboga nyingi na wakati mwingine hutoa bure kwa majirani. Kwa siku ninauza angalau trei tatu za mayai kwa zaidi ya Sh1,200. Hivi karibuni nitaanza kufuga nguruwe hapa nyumbani,” Muiruri anaarifu.

Kwake Muiruri, uthabiti wake kibiashara unajikita katika kugeuza changamoto kuwa nafasi ya kupata ufanisi.

Muiruri anatoa changamoto kwa watu wanaoishi na ulemavu wajitokeze kukumbatia nguvu zao kwa sababu ulemavu si kutojiweza.

  • Tags

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Ni Kamishna Msaidizi aliye pia muundaji wa...

KILIMO: Anapigiwa mfano kwa kuleta ukuzaji mzuri wa mboga

T L