• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
UJASIRIAMALI: Ni Kamishna Msaidizi aliye pia muundaji wa matofali

UJASIRIAMALI: Ni Kamishna Msaidizi aliye pia muundaji wa matofali

NA PETER CHANGTOEK

DAWIN Orina amekuwa akitengeneza matofali kwa muda wa mwongo mmoja na nusu sasa. Yeye ni Kamishna Msaidizi wa kaunti ndogo ya Nyakach, Kaunti ya Kisumu.

“Nilianza kutengeneza matofali 2007, baada ya vita vilivyotokea baada ya uchaguzi. Nilijifunza kutoka kwa wazazi wangu waliokuwa wakiyatengeneza, japo kwa kiasi kidogo ikilinganishwa na wakati huu,” asema Orina, mwenye umri wa miaka 29.

Anafichua kuwa alianzisha shughuli hiyo kwa kuutumia mtaji usiopita Sh10,000.

Anaongeza kwamba, alikuwa akiyatengeneza matofali baada ya kutoka shuleni na nyakati za wikendi.

Orina, ambaye amekuwa akiendeleza shughuli hiyo katika eneo la Cherangany, Kaunti ya Trans Nzoia, ana wafanyakazi watatu wa kudumu na saba wanaomsaidia katika shughuli hiyo, wakati kazi inapokuwa kubwa.

“Ninapokuwa kazini, huwasiliana na mfanyakazi wangu mmoja mwaminifu. Wakati mwingine huenda nyumbani ili kuangalia jinsi shughuli inavyoendelea,” asema.

Orina, ambaye huutumia udongo wa mfinyanzi kuyatengeneza matofali, anasema kuwa, ana wateja wengi anaowauzia, na wakati mwingine huwauzia wakandarasi.

Huyauza kwa kati ya Sh8 na Sh15 kila moja, kwa kutegemea saizi, na wateja wenyewe. Hupata malighafi kutoka kwa wenyeji wa eneo hilo.

Hata hivyo, anasema kuwa kuna changamoto kadha wa kadha ambazo amezipitia katika shughuli hiyo.

Miongoni mwa ndaro hizo ni pamoja na ukosefu wa hela za kutosha za kuendeleza shughuli hiyo. Aidha, ukosefu wa wafanyakazi wa kutosha na malighafi, ni shida nyingine anayosema amepitia.

Isitoshe, mfumukobei huathiri biashara yake.

“Nina wateja wengi, ndiposa huwa yanatakikana kwa wingi katika miezi ya Aprili na Desemba,” afichua Orina.

Anadokeza kwamba, matofali yanayotengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi ni bora ikilinganishwa na mawe kwa sababu mawe huuzwa kwa bei ghali.

Yeye huyatengeneza matofali yaliyo na vipimo tofauti tofauti kuambatana na matakwa ya wateja wake. Hata hivyo, yaliyo na ukubwa wa sentimita 8 kwa 4 kwa 6, ndiyo yanayoagizwa sana na wateja.

“Ninawasihi watu wajitose katika biashara hii, hususan wale ambao hawana kazi. Nimefanya mengi kupitia kwa biashara hii. Pia, si lazima waende kusomea shughuli hii ili kuanza kuifanya,” ashauri Orina, ambaye kwa sasa ana matofali zaidi ya 20,000 yaliyo tayari kuuzwa.

“Sijawahi kuwa na nia ya kuacha shughuli hii, lakini nina nia ya kununua mashine ya kisasa, ili kupanua biashara na kutengeneza nafasi za ajira kwa vijana wenzangu,” asema.

  • Tags

You can share this post!

Siri ya ufugaji nyuki ipo katika uongezeaji thamani

UFUGAJI: Ulemavu kwake si kikwazo, umempa nguvu ya kujituma

T L