• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Ratiba ya kudurusu nyumbani kwa wanafunzi

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Ratiba ya kudurusu nyumbani kwa wanafunzi

Na MARY WANGARI

KATIKA makala iliyopita, tuliangazia kuhusu vigezo muhimu vya kuzingatia wakati mwanafunzi anapounda ratiba ya kusomea nyumbani wakati wa likizo au mapumziko yoyote.

Kando ni kwamba wakati wa likizo hutoa fursa muhimu ya mapumziko kwa wanafunzi, umuhimu wa kuwa na ratiba ya kuwezesha kudurusu nyumbani hauwezi ukasisitizwa vya kutosha.

Mwanafunzi yeyote anayetaka kutia fora katika masomo yake hususan wanafunzi wanaojiandaa kwa mitihani ya kitaifa kama vile KCPE na KCSE, kukosa ratiba ya nyumbani ni sawa na kujichimbia kaburi mwenyewe.

Ni vyema kusisitiza kuwa kuunda ratiba pekee hakutakuwa na maana au umuhimu wowote endapo mwanafunzi husika atakosa nidhamu ya kuiheshimu na kuizingatia.

Iwapo mwanafunzi atachukua muda wake na kutengeneza ratiba ambayo anafahamu vyema hana nia ya kuzingatia, basi ratiba yenyewe itasalia kuwa pambo tu badala ya nyenzo muhimu ya masomo.

Jinsi ya kuandaa ratiba ya nyumbani na umuhimu wake

Ratiba ya kusomea nyumbani si lazima iwe wakati wa likizo lakini inaweza kutumika hata baada ya shule kufunguliwa.

Mwanafunzi anapounda ratiba ya kusomea nyumbani, ni muhimu kupanga masomo ya siku itakayofuata na kuyajumuisha katika ratiba ya somo la siku husika.

Kufanya hivyo kutamsaidia mwanafunzi kudurusu mada au somo lililotangulia pamoja na vipengele vyake.

Aidha, kutamwezesha mwanafunzi kuwa tayari endapo mwalimu ataamua kuleta jaribio la ghafla la kufungua muhula au hata majaribio ya kuendeleza masomo katika muhula (CATs).

Ni wazi kwamba wanafunzi wenye tabia ya kudurusu mara kwa mara huwa na wakati rahisi wanapofanya mitihani au majaribio anuai.

Isitoshe, kando na kumwezesha mwanafunzi kuelewa vyema mada aliyofunzwa, kudurusu vilevile kumpa mwanafunzi ufahamu fulani wa mada mpya inayotangulizwa na mwalimu siku inayofuata hivyo kufanya iwe rahisi kuelewa.

Umuhimu mwingine wa ratiba ya kusomea nyumbani ni kuwa, humwezesha mwanafunzi kufanya mapitio ya kutosha kwa mada za awali.

Kufanya hivi kutamsaidia ama kujibu au kuuliza maswali mbalimbali kuhusu mada iliyotangulia, yanayoulizwa na mwalimu katika juhudi za kupima uelewa wa wanafunzi wake kuhusu mada husika.

You can share this post!

Haaland awabeba Dortmund dhidi ya Wolfsburg katika...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Jinsi ya kuandaa ratiba ya...