• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Haaland awabeba Dortmund dhidi ya Wolfsburg katika Bundesliga

Haaland awabeba Dortmund dhidi ya Wolfsburg katika Bundesliga

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Erling Braut Haaland alifunga mabao mawili na kusaidia Borussia Dortmund kuwakomoa VfL Wolfsburg 2-0 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo Jumamosi.

Ushindi huo uliwezesha Dortmund waliomaliza mechi hiyo na wachezaji 10 uwanjani kuweka hai matumaini ya kukamilisha kampeni za Bundesliga msimu huu ndani ya orodha ya nne-bora ili kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Chipukizi Jude Bellingham alionyeshwa kadi nyekundu kwa mara ya kwanza katika taaluma yake ya usogora baada ya kumchezea visivyo Kevin Mbabu katika dakika ya 59.

Mabao mawili yaliyopachikwa na Haaland kimiani kunako dakika za 12 na 68, yalifikisha idadi ya magoli yake kufikia sasa msimu huu kuwa 25.

Ina maana kwamba nyota huyo raia wa Norway sasa amefunga jumla ya mabao 16 ugenini kufikia sasa muhula huu. Ni ufanisi uliomwezesha kuvunja rekodi iliyowekwa na fowadi Pierre-Emerick Aubameyang kambini mwa kikosi hicho mnamo 2016-17.

Dortmund kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano jedwalini kwa alama 55, moja pekee nyuma ya Eintracht Frankfurt wanaofunga orodha ya nne-bora. Wolfsburg wanashikilia nafasi ya tatu kwa pointi 57, nne nyuma ya RB Leipzig wanaokamata nambari ya pili.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Jinsi janga la Covid-19 lilivyochangia kuongezeka kwa visa...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Ratiba ya kudurusu nyumbani kwa...