• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
ULIMBWENDE: Unachotakiwa kufahamu kabla ya kutumia vipodozi, marashi

ULIMBWENDE: Unachotakiwa kufahamu kabla ya kutumia vipodozi, marashi

Na MARGARET MAINA

[email protected]

AGHALABU watu wengi wana mazoea ya kutumia marashi na vipodozi mbalimbali katika ngozi zao kwa malengo mbalimbali kama vile kunukia vizuri, kuondoa kitu fulani au kuimarisha mwonekano.

Baadhi hununua vipodozi hivi kwa mazoea iwe kwa kuambiwa au kushauriwa na daktari.

Makosa yaliyozoeleka ni baadhi kusahau kusoma lebo au hata kutoona umuhimu wa kufanya hivyo kwa sababu tu kipodozi kimojawapo kimemsaidia mtu fulani au umeshauriwa na mtaalam hivyo unadhani hakina madhara.

Ni muhimu kusoma lebo ili kujua mambo yafuatayo:

Kujua viungo kwenye kipodozi

Ni muhimu kujua kipodozi unachokitumia kina viungo gani na kama ni salama kwa ngozi yako. Ifahamike kwamba kwenye vipodozi, huwa wanaweka kemikali mbalimbali na nyingine ni kali zinazoweza kukusababishia madhara baadaye.

Inawezekana tusiwe wazuri sana kwenye haya mambo ya kusoma kuhusu kemikali ila tufahamu kuna mitandao ya kutuelimisha. Jaribu kutafuta mtandaoni ili uone maelezo ya vitu vilivyotumika katika utengenezaji wa kipodozi husika.

Siku ya kuharibika

Ni muhimu kujua kipodozi chako kinaisha muda wake wa kutumika lini. Baada ya muda wa kipodozi kuisha inawezekana kisilete matokeo mazuri au pia huenda kikakuletea madhara katika ngozi yako.

Namna ya kukihifadhi kipodozi chako

Kwenye lebo huwa kuna maelezo ya namna kipodozi chako kinavyofaa kuhifadhiwa. Unaweza kuambiwa kisikae juani, kiwekwe sehemu ambapo joto lake ni kiasi fulani miongoni mwa mengine. Hivyo ni muhimu kujua haya yote ili kupata matokeo mazuri ya kipodozi katika ngozi yako.

Namna ya kukitumia

Kwenye lebo, kuna maelezo kama unaweza kukuta kimeandikwa kitumiwe mara mbili kwa siku kama vile asubuhi na wakati wa kulala. Vingine hutakiwi kulala navyo, lakini pia kuna vile ambavyo unaambiwa utumie moja kwa moja kwenye tatizo kama kupaka sehemu iliyo na chunusi au doa tu bila kupaka kwingineko ambako hakuna madhara. Ni muhimu kujua haya yote.

Msimu wa kupaka kipodozi chako

Kuna vipodozi ambavyo huwa vinapakwa kwa msimu, labda wakati wa baridi au joto. Inabidi ujue kipodozi unachokitumia kinafaa kutumika katika msimu au hali gani ya hewa, japo si vipodozi vingi ambavyo huandikwa lakini unaweza kujua kwa kusoma viungo au malighafi ambayo ni sehemu ya kipodozi na hali zinazofaa.

You can share this post!

Warembo na ganda la chungwa

Uingereza kigezoni wakijiandaa kuvaana na Ukraine kwenye...