• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
USHAURI NASAHA: Hakikisha una mwanzo mzuri na imara katika ngazi mpya masomoni

USHAURI NASAHA: Hakikisha una mwanzo mzuri na imara katika ngazi mpya masomoni

NA HENRY MOKUA

KILA mara jambo jipya huzua uchangamfu unaofungamana na wasiwasi wa namna fulani.

Anayelitazamia huvutiwa na wazo kwamba jambo lile litazua changamoto mpya ambazo zaweza kuyakuza maarifa yake.

Pamoja na hilo lakini, huwa na wahaka ikiwa jambo lile litamwendea sawa kama watangulizi wake. Wahaka huu waweza kuwa kiini cha mwanzo mbaya kwa yeyote awaye.

Je, ni hatua gani zinazoweza kuchukuliwa kuhakikisha kwamba mwanafunzi wa gredi ya saba, kidato cha kwanza anakuwa na mwanzo wenye matumaini anapojiunga na ngazi mpya katika elimu yake?

Makaribisho yenye uchangamfu, bashasha ni hatua ya kwanza itakayomfanya mwanafunzi anayeanza katika ngazi mpya kujawa na matumaini. Hii itakuwa hatua muhimu ya kumfanya ajihisi panapostahiki. Hivi ni kwa sababu wapo wengi ambao wamekatiziwa ndoto zao za maisha kwa kupokelewa kana kwamba wamepotea njia. Ijapo kwa mtu mzima, jambo hili laweza kuonekana dogo na lisilo na mashiko, kwa mwanafunzi mwenye umri mdogo vile, hili laweza kuwa tatizo kubwa.

Jambo jingine muhimu ni mashauri ya jumla ya kumnasibisha mwanafunzi huyu mgeni na mazingira yake mapya. Kuelekezwa kuhusu ni wapi pa kufanya jambo fulani na wakati gani ni hatua yenye uzito mkubwa. Shule nyingi hujitahidi kulifanya hili ila zipo miongoni mwazo zisizolitekeleza vilivyo.

Katika kunasibisha huku jambo moja linalohitaji kuwekwa wazi ni kwamba ufanisi ni hakika kwa kila atakayefanya bidii.

Haihalisi kutoa vitisho na kumtia hofu mwanafunzi awaye yeyote yule; hasa zaidi ambaye ndio kwanza anaingia katika ngazi mpya masomoni mwake.

Hatimaye, nidhamu ni muhimu na ili itokee vilivyo, adhabu kwa mwanafunzi yeyote yule yafaa kuwa ya kurekebisha; si kutisha wala kukatiza tamaa.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti yafadhili wanafunzi 738 kuingia sekondari

Kaunti yapigwa breki kuchota mabilioni ya Bandari ya Mombasa

T L