• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Vibabaishi vya mapambano dhidi ya Covid-19

Vibabaishi vya mapambano dhidi ya Covid-19

Na MWANGI MUIRURI

MAPAMBANO dhidi ya wimbi la tatu la mkurupuko wa ugonjwa wa Covid-19 yanahujumiwa na asilimia ya chini ya uhakika kuhusu matokeo ya vipimo.

Imeelezewa kuwa kuna baadhi ya Wakenya ambao wanajitokeza kupimwa kama wameambukizwa virusi vya corona lakini matokeo yanalemewa katika kigezo cha uhakika ambapo wanapatikana hawana virusi hivyo huku baadhi wasio navyo, sampuli zao zikionyesha matokeo chanya kwamba wana maambukizi.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa masuala ya afya katika Kaunti ya Murang’a Dkt Leonald Gikera, ingawa hali hiyo ni ya kawaida katika safu ya vipimo vya kimaabara, bila shaka inatatiza vita dhidi ya virusi hivyo haswa katika kipindi hiki kigumu cha mkurupuko wa tatu tangu Machi 2020.

Alisema kuwa changamoto nyingine ni hali ambapo asilimia 90 ya walio na virusi hivyo bado hawaonyeshi dalili zozote za kuugua na huku kinga yao ya kimwili ikiwa juu, wanatembea katika jamii wakiwa huru huku wakihatarisha maisha ya wengine.

“Asilimia nane ya wanaojitokeza hospitalini baada ya kujihisi kama wanaugua wanaonyesha dalili finyu sana, asilimia mbili tu ikiwa ndiyo inaonyesha dalili za wazi za kuwa na Covid-19,” akasema.

Alisema kuwa hali inafanywa kuwa ya dharura kwa hiyo asilimia mbili kutokana na hali kwamba karibu wote huwa na magonjwa mengine mwilini yanayosambaratisha kinga yao hivyo basi kuwaweka katika hatari kuu ya mauti.

Dkt Gikera alisema kuwa changamoto nyingine ambayo Wakenya wanafaa waelewe ni kuwa wengi wa wagonjwa mahututi wa Covid-19 wakiwekwa katika mitambo ya hali ya dharura (ICU) huishia kuaga dunia.

“Hii ni kwa sababu mikakati ya kuwawezesha kupumua almaarufu intubation huwatatiza kwa kupumua na kuwasababishia mauti ya haraka hivyo basi kimatibabu, wengi wa madaktari hupendelea kuwaweka wagonjwa hao mahututi katika wadi za kawaida lakini zilizo na huduma za karibu sana za wauguzi (HDU),” akasema.

Alisema changamoto hizi zote zinaishia kuwatuma nyumbani walio na virusi vya corona, wengine wakilazwa wakati hawana virusi hivyo huku baadhi ya mauti yakichochewa na mitambo iliyoko katika vyumba vya ICU.

Alisema ubora wa vipimio unafaa kutathminiwa ili kuwepo na asilimia kubwa ya uhakika wa matokeo.

Alisema kuwa kinachohitajika ni vipimio aina tatu ambapo kimatibabu huorodheshwa kama A, B na C.

“Hapa ni pale tukitekeleza vipimo vya kwanza (A) na kwa mfano tupate matokeo ni aliyepimwa ana virusi hivi vya corona, tufanye vipimo vya pili (B) na ambapo ikizuka ako navyo, tutekeleze vipimo vya tatu (C) ndivyo sasa tuelewe kabisa matokeo ya uhakika. Yale matokeo ya awamu ya C ndiyo huwa na uhakika wa asilimia ya juu na ndiyo hutumika kutoa matokeo rasmi,” akasema.

Dkt Gikera alisema kuwa ikiwa vipimio vitaendelea kuwa vya awamu moja tu (A) basi kuna kuchanganyikiwa kwingi ambako kutaendelea kukumba vita dhidi ya janga hili la kiulimwengu ambalo limesababisha vifo vya mamilioni.

Alisema kuwa wale wanaopatikana wakiwa na virusi hivyo katika awamu ya kwanza ya kupima ndio wanaofaa kufanyiwa vipimo vya B na C “kwa kuwa ni suala la kimaadili, kisheria na pia la kisaikolojia kumhukumu asiye na virusi hivyo kuwa ako navyo.

“Aidha, tunaweza tukatumia vipimo hivyo vya kwanza kutambua kuwa ako na virusi lakini kwa uhakika awe hana na tumweke katika malazi sambamba na walioambukizwa hivyo basi tuishie kuhatarisha maisha yake kiasi hata cha kumsababishia mauti. Hii ndiyo sababu inayotutuma tujitahidi kuwa na uhakika wa hali ya juu kabla ya kumuorodhesha yeyote kuwa ameambukizwa,” akasema.

Mkuu wa kitengo cha Afya katika Kaunti hiyo Dkt Winnie Kanyi alisema kuwa changamoto nyingine inazuka wakati wanaojihisi kuwa na Covid-19 wanakimbia kujinunulia madawa katika maduka ya mauzo mitaani bila hata kutekelezewa vipimo vyovyote.

“Hao wanaishia kujitibu bila mwongozo wowote na hatimaye hali inawalemea na kusambaratisha uwezo wao wa kutibiwa hospitalini. Aidha, kunao wanajitokeza katika hospitali za kibinafsi ambapo wanahudumiwa kibisahara na bila kutekelezewa vipimo vyovyote, wanatibiwa magonjwa yasiyo mwilini mwao na katika hali hiyo, ikiwa kwa kweli walikuwa na virusi hivyo, wanahatarisha maisha yao binafsi, ya wengine katika jamii na pia wale wauguzi katika hospitali hizo,” akasema.

Dkt Kanyi alisema kuwa wanaume ndio wako na mazoea ya kusaka matibabu kiholela na pia hungojea hadi walemewe kabisa ndio wasake matibabu wakijipa moyo kwamba mwanamume ni kung’ang’ana.

“Wakati wanang’ang’ana kiume, wanazidisha hatari kwa maisha yao na pia kwa jamii ambapo wanaendelea kuambukiza wengine huku wanaoambukizwa wakiendeleza maambukizi hivyo basi kuunda mtandao mpana wa ugonjwa huu.

Dkt Gikera aidha alisema kuwa ugonjwa huu uko na tabia isiyoeleweka hadi sasa “ambapo mmoja katika familia ataambukizwa na akae na ugonjwa huo hadi umuue, lakini wengine wote waliokuwa wanaishi naye kwa karibu waishie kutoambukizwa.”

Alisema ni hali ambayo imekosa maelezo kimatibabu “kwamba hata utapata mke na mume ambao walikuwa wanashiriki hata tendo la ndoa katika kiitanda kimoja mara kwa mara na mmoja aambukizwe na aage dunia lakini mwenzake apate ako buheri wa afya.”

  • Tags

You can share this post!

Harambee Stars yafika Togo salama salmini

Afisa wa afya wa Nakuru azikwa