• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Harambee Stars yafika Togo salama salmini

Harambee Stars yafika Togo salama salmini

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya soka ya Kenya maarufu kama Harambee Stars ilifika salama salmini Jumamosi usiku nchini Togo kwa mechi ya mwisho ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2022.

Vijana wa kocha Jacob “Ghost” Mulee, ambao waliondoka Nairobi saa tisa alasiri Jumamosi wakitumia ndege ya kukodisha, watapepetana na Sparrow Hawks jijini Lome hapo Machi 29 katika mechi ambayo haina umuhimu kuhusu dimba la AFCON kwa sababu mataifa haya mawili hayatafuzu.

Misri na Comoros zilijikatia tiketi kutoka Kundi G mnamo Machi 25 baada ya kufikisha alama tisa kufuatia sare dhidi ya Kenya na Togo, mtawalia. Kenya na Togo zimezoa alama nne na mbili mtawalia.

Beki Johnstone Omurwa, viungo Anthony ‘Teddy’ Akumu na Kenneth Muguna, ambao walikuwa katika mechi dhidi ya Mafirauni ugani Kasarani, hawapo nchini Togo. Omurwa alionyeshwa kadi nyekundu naye Muguna alipata jeraha. Akumu amejiondoa kutoka safari ya Togo kwa sababu za kifamilia. Sura mpya katika kikosi cha Mulee ni Clyde Senaji ambaye amejaza nafasi ya nahodha wa Gor Mahia, Kenneth Muguna.

Stars inatarajiwa kuwa na kipindi cha mazoezi ugani Kegue hii leo Jumapili kabla ya kumenyana na Togo saa moja usiku saa za Kenya hapo Jumatatu.

Kikosi cha Harambee Stars nchini Togo:

Makipa – Ian Otieno, James Saruni, Joseph Okoth;

Mabeki – Eric Ouma, Joash Onyango, Clyde Senaji, Nahashon Alembi, Harun Mwale, Daniel Sakari, Baraka Badi;

Viungo – Duke Abuya, Cliff Nyakeya, Lawrence Juma, Kevin Simiyu, Duncan Otieno, James Mazembe, David Owino, Kevin Kimani, Abdallah Hassan, Cliffton Miheso;

Washambuliaji – Masud Juma, Michael Olunga (nahodha), Elvis Rupia.

You can share this post!

Utata magavana waliobwagwa wakipanga kuwania

Vibabaishi vya mapambano dhidi ya Covid-19