• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Waislamu Kenya gizani kuhusu kuhudhuria sherehe za hija

Waislamu Kenya gizani kuhusu kuhudhuria sherehe za hija

Na FARHIYA HUSSEIN

WAISLAMU nchini Kenya bado hawajajua ikiwa watakuwa sehemu ya wale watakaohudhuria sherehe za hija za mwaka huu 2021.

Waumini hao bado wanasubiri taarifa rasmi kutoka kwa Baraza Kuu la Waislamu Nchini (SUPKEM).

Zikiwa zimesalia siku 41 tu kwa sherehe hizo kuanza, mawasiliano bado hayajatolewa ikiwa sala takatifu zitahudhuriwa na raia wa Kenya.

Kulingana na Mwenyekiti wa SUPKEM, Hassan Ole Naado, wanasubiri mawasiliano rasmi kutoka kwa Wizara ya Hija na Umrah ya nchini Saudi Arabia.

“Hakuna Mkenya yeyote ambaye amekwenda kwenye sherehe hizo kipindi ambapo tunasubiri mawasiliano rasmi kutoka kwa wizara husika nchini Saudia,” Ole Naado ameambia Taifa Jumapili.

Waislamu kote ulimwenguni watafaa kuanza rasmi sherehe hizo za hija makala ya mwaka huu kuanzia Julai 17 kalenda ya kizungu.

Mahujaji na waswalihina ambao wamepokea chanjo dhidi ya Covid-19 ndio wataruhusiwa kutekeleza sala hizo takatifu, Saudi Arabia imetangaza.

Sherehe za mwaka huu ni za pili kutekelezwa ndani ya kipindi cha janga la corona linaloendelea kuyumbisha matukio mengi duniani.

Hija ni sherehe inayofanyika mjini Mecca, Saudi Arabia mwezi wa Dhul Hijjah ambao ni mwezi wa 12 na wa mwisho katika kalenda ya Kiislamu.

“Mwaka huu mahujaji 60,000 ndio wataruhusiwa kufanya sala takatifu huko Makkah huku 15,000 wakiwa wakaazi wa Saudia. Pfizer na AstraZeneca ni miongoni mwa chanjo zinazozingatiwa. Mahujaji lazima wawe wamekamilisha dozi zote mbili za chanjo ya covid kabla ya kuhudhuria sherehe hizo, ”ilisema taarifa ya Serikali ya Saudi.

Hapo awali, nchi tisa ikiwa ni pamoja na Misri na Afrika Kusini zilisitishwa kutekeleza Umrah, sherehe takatifu inamyofanyika mjini Makka wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Aidha,Wakenya wamehimizwa wasikate tamaa na kujiunga na wengine kwa kusherehekea sala takatifu kupitia shughuli zingine za kidini.

“Ikiwa mtu atakosa nafasi ya kwenda katika mji mtakatifu, Makka kwa sherehe, bado anaweza kufunga, kutoa misaada, kutembelea wagonjwa kati ya shughuli nyingine za kidini,” anasema Kadhi Mkuu Ahmed Muhdhar.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mombasa Covid-19, Sheikh Rishard Rajab anasema mwaka wa 2019, karibu Wakenya 4,500 walihudhuria sherehe hizo za hija.

“Bado hatujapata maelezo kamili kuhusu ni Waislamu wangapi wa kutoka hapa nchini Kenya watakaohudhuria sherehe hizo takatifu mwaka huu. Tunasubiri uthibitisho kutoka kwa SUPKEM,” alisema.

Mwaka 2020, ni wakazi 10,000 tu wa Kiislamu wa Saudi Arabia waliruhusiwa kushiriki kwenye sherehe hizo ambayo ni idadi ya chini mno kulinganishwa na idadi iliyozoeleka ya mahujaji 2.5 milioni wanaofika kutekeleza ibada hiyo kwa kipindi cha kawaida kabla ya janga hilo la Covid-19.

You can share this post!

Nitapigania ugavana tena katika uchaguzi wa 2022 –...

Borussia Dortmund wapunguzia Manchester United bei ya Jadon...