• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:43 AM
Wakulima wa kahawa wahimizwa kuchukua mikopo isiyotozwa riba

Wakulima wa kahawa wahimizwa kuchukua mikopo isiyotozwa riba

NA SAMMY WAWERU

WAKULIMA wa kahawa nchini wamehimizwa kuchukua mikopo isiyotozwa riba ili kupunguza gharama ya uzalishaji.

Meneja wa New KPCU, Bw Timothy Mirugi ameiambia Taifa Leo serikali imetenga kima cha Sh3 bilioni kupiga jeki wakulima wa kahawa.

Mgao huo ulitolewa mwaka uliopita, 2021.

Afisa huyo alisema Sh151 milioni pekee ndizo zimesambazwa kufikia sasa.

Alisema wakulima wanachelea kuchukua fedha hizo, kwa kile alitaja kama “wengi kutokuwa na ufahamu”.

“Kiwango cha uchukuaji ni cha chini, wengi hawafahamu watakavyopata mkopo huo,” Bw Mirugi akasema.

Wakulima wa kahawa wanalalamikia mfumko wa bei ya fatalaiza, hatua wanayosema inatishia uzalishaji wa kiungo hicho cha kunywa.

Kwa sasa, mfuko wa kilo 50 umepanda bei zaidi ya mara dufu. Mwaka wa 2020, ulikuwa ukiuzwa Sh2, 500.

Hii ina maana kuwa ongezeko hilo limeshuhudiwa chini ya kipindi cha muda wa miaka miwili pekee.

Ongezeko hilo la bei ya mbolea, ambalo linakumba sekta ya kilimo kwa jumla, ni kero ya kimataifa hasa baada ya mkurupuko wa janga la corona.

Malighafi yanayotumika kutengeza mbolea yamepanda bei. Kenya huyategemea kutoka nchi za nje kuunda mbolea.

Huku New KPCU ikiwataka wakulima wa kahawa kuendea fedha walizotengewa na serikali ili kuboresha ukuzaji, taasisi hiyo inafanya hamasisho kupitia viwanda na vyama vya ushirika.

“Ni fedha zao, waje wazichukue ili wapunguze gharama ya juu ya uzalishaji wa kahawa,” Mirugi akahimiza.

Alidokeza kwamba, mkopo huo unatozwa ada ya asilimia 3 pekee, mara moja.

Dhamana, ni mazao ambayo wakulima husambazia shirika hilo linalojukumika kuyatafutia soko.

New KPCU inafanya kazi na zaidi ya wakulima 50, 000 wa kahawa.

Rais Uhuru Kenyatta 2019 alifanya mabadiliko ya taasisi ya zamani, KPCU kufuatia uongozi mbaya uliokuwa ukishuhudiwa, ambapo aliagiza kubuniwa kwa New KPCU.

Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya amekuwa akiendeleza mageuzi katika shirika hilo la kahawa.

Licha ya soko kuboreka na wakulima kukiri kupata mapato ya kuridhisha, wanateta yanaishia kununua mbolea.

Kiwango cha uzalishaji wa kahawa Kenya kimepungua, ikilinganishwa na miaka ya hapo awali.

  • Tags

You can share this post!

Wanajeshi wa KDF waua wapiganaji wanne wa al-Shabaab...

Canada yazima ndege za Urusi katika anga yake

T L