• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Walilia vijana kupiga Raila jeki kwa kujisajili kura

Walilia vijana kupiga Raila jeki kwa kujisajili kura

Na GEORGE ODIWUOR

WASHIRIKA wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, wamewalilia vijana wa Nyanza na Mlima Kenya, wakiwataka wamsaidie Bw Odinga kuingia Ikulu 2022 kwa kujiandikisha kwa wingi kuwa wapiga kura.

Wabunge Gladys Wanga (Mbunge Mwakilishi wa Kike Homa Bay), mwenzake wa Murang’a Sabina Chege, Charles Njagagua (Mbeere Kaskazini) na Martin Owino (Ndhiwa), walisema vijana kutoka maeneo hayo mawili ndio wenye kura nyingi za kumwezesha Bw Odinga kushinda urais.

Walisema maeneo hayo mawili yana idadi kubwa ya kura ambazo zitaweza kumsaidia waziri huyo mkuu wa zamani kufikia ndoto yake ya kuwa Rais wa Kenya 2022.Bi Chege alisema amekuwa akimpigia debe Bw Odinga katika kaunti yake na wapiga kura huko wamemhakikishia kuwa wako tayari kumpigia kura kiongozi huyo wa ODM kwa kujiandikisha kuwa wapiga kura.

Akiongea katika Kaunti ya Homa Bay Ijumaa, Bi Chege hata hivyo alisisitiza kuwa vijana wa Nyanza pia wanafaa kuiga wenzao wa Mlima Kenya kwa kujiandikisha kwa wingi.“Wakenya wengi wanataka amani kuendelea kudumu nchini Kenya baada ya uchaguzi mkuu ujao.

Kwahivyo, wapiga kura, haswa vijana wa Nyanza, sharti wawe tayari kushirikiana na wenzao wa eneo la Kati ili kuendeleza moyo wa handisheki 2022,” Bi Chege akaeleza.“Kwa hivyo, sharti Wakenya wachague kiongozi ambaye ataunga mkono ajenda ya amani.

Na huyo si mwingine ila ni Raila Odinga,” akaongeza.Bi Chege ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya, alisikitika kuwa idadi ndogo ya watu wanaojiandikisha kuwa wapiga kura katika eneo la Nyanza, huenda ikamnyima kiongozi huyo wa ODM nafasi ya kuingia Ikulu.

“Sharti vijana katika eneo hili wafahamu kuwa idadi ya wapiga kura ni suala muhimu zaidi katika uchaguzi. Kwa hivyo, mjiandikishe kwa wingi ili kuendeleza ajenda ya handisheki baada ya 2022,” akasema alipoongoza uzinduzi wa mashindano ya kandanda ya Wanga Genowa, katika shule ya msingi ya Okok, wadi ya Kologi, eneo bunge la Ndhiwa, Homa Bay.

Mwenyeji wake, Bi Wanga, alisema kuwa afisi za wabunge kutoka Nyanza zimeweka mipango ya kuchukua vitambulisho vilivyopokwa afisi za usajili na kuvisambaza kwa wenyewe.Alisema vitambulisho vya kitaifa vinafaa kutayarishwa kwa muda mfupi ili kuwezesha vijana kujiandikisha kuwa wapiga kura.

“Shida kuu inayoathiri watu wetu ni muda mrefu kati ya wakati mtu anapotuma ombi la kitambulisho na wakati stakabadhi hiyo inapokuwa tayari. Afisi yangu na zile za wenzangu katika eneo hili, zinasukuma shughuli hii kwa sababu tunataka watu wote washiriki upigaji kura,” Bi Wanga akasema.

Kauli yake iliungwa mkono na Bw Owino ambaye alisema afisi yake pia imeshirikisha wahudumu wa afya katika jamii kutambua watu ambao hawajapokea vitambulisho vyao na kujiandikisha kuwa wapiga kura.

Kwa upande wake, Bw Njagagua aliwashauri vijana kuwa kwa kupiga kura wataweza kuchagua viongozi wanaowataka na ambao watatekeleza maendeleo wanayotaka.Shughuli hiyo pia ilihudhuriwa na Mbunge wa Keiyo Kaskazini, Dkt James Murgor ambaye anatoka katika ngome ya Naibu Rais William Ruto ambaye ni mpinzani mkuu wa Bw Odinga.

You can share this post!

K’Ogalo juu ya meza Tusker wakionja ushindi wa kwanza

Wakazi walia kucheleweshewa soko

T L