• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Wanabodaboda walia abiria wa kike kuwaweka majaribuni kimapenzi

Wanabodaboda walia abiria wa kike kuwaweka majaribuni kimapenzi

KNA NA GEORGE ODIWUOR

WAHUDUMU wa bodaboda kutoka Kaunti ya Mombasa, wamelalamika wakidai kuwa, baadhi ya abiria wao wa kike huwadhulumu kingono.

Wakizungumza katika mkutano wa idara ya kitaifa inayoshughulikia masuala ya jinsia, walitaka juhudi za serikali kupambana na dhuluma za kingono katika jamii ziangazie pia yale ambayo wao hupitia.

Mkutano huo ulilenga kuhamasisha waendeshaji bodaboda hao kuhusu dhuluma za kijinsia na pia kuanzisha mijadala kuhusu njia chanya kuwawezesha wanaume kubadilisha mtazamo kuhusu unyanyasaji.

Wahudumu hao walimweleza Mkurugenzi wa Idara ya kupambana na dhuluma za kijinsia, Bi Halima Abdi, kwamba walikuwa wakitatizika na dhuluma kutoka kwa abiria wao wakiwa kazini.

“Kama mwendeshaji bodaboda, tunakumbana na changamoto nyingi sana hasa zile zinazotudhulumu kijinsia. Mara nyingi tukisikia unyanyasaji wa kijinsia tunajua tu unawakumba wanawake, ila hata sisi wanaume tunakumbana na unyanyasaji,” akasema Katibu Mkuu wa kikundi cha waendeshaji bodaboda Kaunti ya Mombasa, Bw Josphat Oduor.

Alidai kuwa, baadhi ya wanawake hutumia mahaba kama njia ya kutotaka kuwalipa wahudumu wa bodaboda wanapowasafirisha.

“Wakituona, wanajua ni nafasi ya kusafirishwa bila kulipa pesa. Ukieleza unataka kulipwa wanasema watajitolea kushiriki nawe tendo la ndoa kama malipo. Hata hulka zao huwa zinaonyesha kuwa kuna nia fiche hasa tunapofanya kazi usiku,” akasema Bw Oduor.

Kwa mujibu wa waendeshaji hao, kulikuwa na umuhimu wa hamasisho kuhusu masuala hayo, wakieleza kuwa walipata ufahamu wa kuwepo kwa dawati la kuripoti visa vya dhuluma za kijinisa katika vituo vya polisi.

“Zamani hakukuwa na madawati haya. Tulikuwa tukienda kuripoti visa hivi unachekwa kama mwanamume,” akasema Bw Oduor.

Kwa miaka mingi, wahudumu wa bodaboda wamekuwa wakilaumiwa kwa utovu wa nidhamu ikiwemo unajisi wa wasichana wa shule, na aina nyingine za uhalifu.

Hata hivyo, baadhi yao wameanza kuchukua hatua kujiondolea sifa mbaya ambayo imekuwa ikiwaandama.

Mwenyekiti wa Muungano wa usalama wa waendesha bodaboda, Bw Kevine Mubadi, ni miongoni mwa waendeshaji, wanaoendeleza kampeni hizo kuipa umma imani kwa wahudumu hao.

“Waendeshaji bodaboda wamekuwa wakijulikana kama watu wanaoongoza maandamano na mambo mengine ambayo ni kinyume cha sheria. Hili si kweli na tunataka kufanya mabadiliko kwa kuwasajili waendeshaji kwa makundi ya kuwawezesha kiuchumi,” akasema.

Kulingana naye, kujiunga na makundi na hata mashirika kutawawezesha kutafuta njia mbadala za kujipatia riziki kando na kuwa barabarani wakiwasubiri wateja.

Kwa mujibu wa Bw Mubadi, serikali kupitia wizara ya usalama wa ndani imewaunga mkono kwa hamasisho wanazoendeleza, ili kubadilisha mtazamo wa biashara hiyo muhimu.

Bw Mubadi aliwaomba wanabodaboda kutoka sehemu mbalimbali za humu nchini kutotumika na wanasiasa kutekeleza mahitaji yao.

“Kadri tunapoongeza juhudi za kusafisha jina letu kwa umma kuna wale bado wanaturejesha nyuma. Ninawaomba endapo tutahusika na wanasiasa isiwe juu ya mambo mengine bali tu suala la maendeleo yanayotuhusu,” akasema alipohudhuria uchaguzi wa viongozi wa bodaboda eneo la Mbita, ambako Bw Fredrick Odhiambo alichaguliwa mwenyekiti wa waendeshaji bodaboda katika eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

Azimio wapendekeza Mwenje awe naibu kiranja wa wachache...

Gaspo Women kuzuru TZ na Uganda kwa mechi za kirafiki

T L