• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Wanafuga samaki wa kiume pekee kufungia nje ushindani

Wanafuga samaki wa kiume pekee kufungia nje ushindani

NA PETER CHANGTOEK

KATIKA umbali wa kilomita takribani 60 kutoka jijini Nairobi, shamba moja la ufugaji samaki linatambulika kwa wengi. Kamuthanga Fish Farm, shamba linalojulikana kwa ufugaji wa samaki kwa kutumia teknolojia ya kisasa, linapatikana katika eneo la Mua Hills, Kaunti ya Machakos.

Anthony Ndeto ni mmiliki wa shamba hilo, ambalo ni la kwanza katika eneo la Afrika Mashariki na Kati kuidhinishwa na kukabidhiwa cheti cha ARSO (African Organisation for Standardisation) 2019.

Ndeto alijitosa katika ufugaji wa samaki 2013. Shamba lote ni ekari tano na lina sehemu ya kuwazalisha samaki wa kiume kwa kuitumia teknolojia inayojulikana kama super male ama YY.

Teknolojia hiyo ni ya kuwazalishia samaki wa kiume pekee. Hapo awali, samaki walikuwa wakizalishwa wakitumia homoni ambazo zinageuza jinsia ya samaki wa kike kuwa wa kiume.

Hata hivyo, meneja wa kitengo cha samaki katika shamba hilo, Joseph Odhiambo, anasema kuwa, waliacha kutumia homoni, na kwa wakati huu huleta mbegu za samaki kutoka Uholanzi.

Wakati walipokuwa wakianza, hawakuwa wakizalisha samaki kwa kiwango cha juu sana, na walipitia changamoto kadhaa. Hata hivyo, walianza kushirikiana na shirika la FoodTechAfrica, shirika kutoka Uholanzi.

“Wakati ushirikiano huo ulipoanza 2014-2018, shamba hili likawa na uwezo wa kuzalisha mara thelathini zaidi, kwa sababu kwa wakati huo tulikuwa tukivua samaki chini ya kilo 5,000 kwa mwaka, na kwa wakati huu, tunaweza kupata samaki tani 100,” asimulia Odhiambo, ambaye amefanya kazi kwa shamba hilo kwa muda wa takribani miaka minane.

Joseph Odhiambo akifafanua kuhusu teknolojia ya kuzalisha samaki wa kiume pekee, ijulikanayo kama YY. PICHA | PETER CHANGTOEK

Mwanzoni, walikuwa wakitumia vidimbwi vilivyokuwa katika maeneo yaliyokuwa wazi, lakini kwa wakati huu, hutumia majengo makubwa yaliyo na matangi 50. Matangi hayo yalijengwa kwa kutumia saruji.

“Kila tangi lina maji lita 50,000. Kila moja hutoa tani 3,000 za samaki. Karibu nusu yao yanatumika kwa sasa, lakini tuna mipango ya kuhakikisha kuwa yote yanatumika. Tunawafuga samaki 20,000 kwa nafasi ndogo ya mita tano mraba yenye kina cha futi mbili na nusu. Huwalisha kila baada ya saa mbili; usiku na mchana,” aeleza Odhiambo.

Odhiambo anasema kuwa, kwa kawaida katika ufugaji wa samaki, watu huruhusiwa kuwafuga samaki wanne kwa sehemu iliyo na ukubwa wa mita moja mraba, lakini kwa teknolojia hii, imewawezesha kuwafuga samaki 135 kwa mita moja mraba.

Anasema kuwa, maadamu wanatumia majengo makubwa yanayofanana na vivungulio, wana uwezo wa kudhibiti hali ya hewa ndani, na hivyo kuwa na uwezo wa kuzalisha kila wakati pasi na kukosa kuwawasilisha sokoni.

Iwapo halijoto ziko chini, uzalishaji huchukua muda mrefu sana, ilhali wakati halijoto zinapokuwa juu, samaki hukua haraka mno.

“Tuna lori ambalo huwasafirisha samaki walio hai sokoni. Sisi pekee ndio tunaowauza samaki hai katika eneo la Nairobi,” asema meneja huyo, akiongeza kuwa, lengo kuu kwao ni kuwauza samaki walio hai sokoni.

Anaongeza kuwa, wakulima wengi hupenda kuwafuga samaki wa kiume kwa sababu hukua upesi, ikilinganishwa na samaki wa kike, na hivyo wao hupata hela haraka kwa kuwafuga wa kiume.

Odhiambo anafichua kuwa, wao huzinunua lishe kutoka nchini Misri kwa sababu si ghali na ni za kiwango cha juu.

Changamoto kuu kwao ni gharama ya juu ya uzalishaji. Changamoto nyingine ni bili za juu za stima. Anasema kuwa uuzaji wa samaki kutoka China, pia, huwaathiri wafugaji wa humu nchini, na hivyo serikali inafaa kuliangazia suala hilo.

Hata hivyo, anasema kuwa, samaki wao hawawezi kulinganishwa na wale wanaoletwa kutoka China, kwa sababu wanaoletwa kutoka China huwa wamekaushwa, ilhali wanaozalishwa katika shamba la Kamuthanga Fish Farm, huuzwa wakiwa hai.

Kwa wakati huu, shamba hilo lina wafanyakazi 13 kwa idara ya samaki, na kwa kuwa kuna shughuli nyingine za kilimo shambani kama vile ufugaji wa nguruwe, kuku na ukuzaji wa mimea ya mboga, wafanyakazi wote wanaweza kufikia 40 kwa idadi.

Odhiambo anafichua kuwa, Kamuthanga Fish Farm inapania kuongeza kiwango cha uzalishaji maradufu ifika 2025.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wa kike washauriwa waungane kuboresha maisha

Ukur Yatani atisha kumshtaki Nyakang’o

T L