• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:07 PM
WANDERI KAMAU: Buriani mhariri wetu mahiri Mauya Omauya

WANDERI KAMAU: Buriani mhariri wetu mahiri Mauya Omauya

Na WANDERI KAMAU

HUJAMBO msomaji?

Kwa kawaida, nafasi hii huwa ya mwandishi Mauya Omauya kila Ijumaa, ambapo huwa anaandika makala kuhusu masuala mbalimbali kama siasa, historia, falsafa na mahusiano ya kimataifa.

Hata hivyo, nina moyo mzito kuandika makala haya kumhusu, kwani hayupo nasi tena duniani. Bw Mauya alifariki Jumatatu katika mtaa mmoja jijini Nairobi baada ya kuzimia ghafla.

Ripoti ya upasuaji wa mwili wake ilionyesha alifariki kutokana na matatizo ya moyo.

Wakati wa kifo chake, Bw Mauya alikuwa mhadhiri wa masuala ya mawasiliano na mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Moi.

Alikuwa na shahada ya uzamili katika Mahusiano ya Masuala ya Kimataifa kutoka chuo cha School of African Oriental Studies (SOAS), London, Uingereza.

Kando na kuwa mwanahabari, alikuwa msomi, mwandishi na mhariri maarufu, ambapo kando na magazeti ya Kenya, alikuwa akichambua siasa katika magazeti ya kimataifa kama China Daily.

Kama msomi barobaro, kifo chake ni pigo kubwa kwa tasnia ya uanahabari na usomi nchini.

Kwa muda ambao nilitangamana naye – kati ya 2013 na 2014 – Bw Mauya alidhirisha uelewa mpevu na wa kipekee kuhusu matukio mbalimbali duniani.

Kama msomi, hungemkosa bila kitabu ama kijarida. Alivipenda, akivitaja kuwa “chemichemi na mwanzo wa kuifahamu dunia.”

Bw Mauya pia alikuwa mpenzi mkubwa wa muziki aina ya Rhumba na waandishi wa Kiafrika.

Katika maandishi yake, hangekosa kumnukuu mwandishi Chinua Achebe, hasa novela ya ‘Things Fall Apart’ (Mambo Huangamia).

Alishikilia kuwa waandishi wa fasihi ya Afrika ndio walioifahamisha dunia nzima kuwahusu Waafrika – tamaduni zao, siasa zao na mpangilio wa kijamii.

Kutokana na imani yake kubwa kuhusu Uafrika, ukombozi na mustakabali wake, alikuwa na mazoea ya kuvaa kijikofia kilichovaliwa na wanasiasa maarufu kama vile Mzee Jomo Kenyatta, Jaramogi Oginga Odinga, Kwameh Nkrumah kati ya wengine.

Sifa yake nyingine ni kwamba alikuwa mpenzi mkubwa wa muziki wa Reggae.

Aliwapenda wanamuziki walioimba nyimbo zenye maudhui ya ukombozi wa Mwafrika kama Bob Marley, Peter Tosh, Lucky Dube, na Joseph Hill (Mighty Culture).

Mkasa mkuu katika maisha yetu ni kwamba kifo ni sehemu ya matukio tutakayokumbana nayo, kulingana na mwandishi Haruki Murakami kutoka Japan.

Ingawa kifo kimekuwa kikionekana kama mkasa katika maisha ya mwanadamu, imebidi tukubali uhalisia wake, kwani ni njia inayopitiwa na kila kiumbe aliye hai.

Kifo huliza na huatua moyo. Huwa kinavuruga mipango na mielekeo ya maisha yetu. Ni adui tusiyemwepuka hata kidogo.

Tulipotangamana naye akiwa mhariri, alinichochea sana kurudi chuoni kujikuza kimasomo kutokana na ufahamu mpevu aliokuwa nao kuhusu siasa za kimataifa.

Licha ya kuondoka baada ya kuhudumu kama mhariri, tuliendelea kutangamana naye, hasa mitandaoni, nikimwomba mwongozo kuhusu masuala mbalimbali ya kiakademia.

Kama mwalimu na mwanafunzi wake, Bw Mauya alikuwa mwenye roho safi, mjalifu, mwenye huruma na mpenda watu.

Daima, hakujiweka kwenye hadhi ya kiusomi, bali alikuwa tayari kuzungumza na kucheka na yeyote aliyekuwa karibu naye.

Ni Mungu hutoa na ndiye huchukua. Tutamkumbuka daima. Mola amlaze penye wema. Amin.

[email protected]

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Hali ya corona India ni tisho kubwa,...

Wasanii wa Baba Dogo watikisa anga za muziki jijini