• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
BENSON MATHEKA: Hali ya corona India ni tisho kubwa, tusilegeze kamba

BENSON MATHEKA: Hali ya corona India ni tisho kubwa, tusilegeze kamba

Na BENSON MATHEKA

RIPOTI za kiwango cha maambukizi ya virusi vya corona nchini India zinatisha. Watu wanakufa kwa wingi katika nchi hiyo ya pili kwa idadi ya watu ulimwenguni.

Hali hii imesababishwa na ukiukaji na mapuuza ya kanuni za kuzuia msambao wa virusi hivyo hatari vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Hospitali katika nchi hiyo, iliyo na moja ya mifumo thabiti ya afya ulimwenguni, zimelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa. Wagonjwa wengi wanakosa vitanda vya wagonjwa mahututi na pia hewa ya oksijeni kuwasaidia kupumua.

Tanuri za kuchomea maiti zimekumbwa na uhaba wa kuni kufuatia kuongezeka kwa idadi ya watu wanaofariki sababu ya corona.

Yanayoendelea India yamezua wasiwasi kote ulimwenguni ikizingatiwa kuwa nchi nyingi, hasa barani Afrika na Amerika Kusini, huitegemea kwa dawa, vifaa na teknolojia za matibabu.

Tayari, shughuli ya utoaji wa chanjo ya corona inatishiwa baada ya nchi hiyo kusitisha uuzaji wa chanjo ya Astrazeneca, iliyokuwa ikipelekwa katika mataifa mengine, ili kukithi mahitaji nchini humo.

Ni muhimu kwa nchi nyingine ulimwenguni kufahamu kilichosababisha mlipuko wa wimbi la pili na hatari la corona nchini India, ambayo ilikuwa imepunguza maambukizi.

Mapema mwaka huu, serikali ya India ililegeza masharti ya kuzuia msambao wa virusi hivyo kwa kuruhusu raia kushiriki sherehe za kila mwaka za kidini.

Watu walitangamana na kusongamana katika maeneo matakatifu ya nchi hiyo kwa sherehe hizo bila kuvalia barakoa. Vile vile, katika baadhi ya majimbo ya nchi hiyo, serikali iliruhusu kampeni za uchaguzi kufanyika.

Kulikuwa pia na maandamano makubwa ya wakulima waliokuwa wakilalamikia sera mpya ya Waziri Mkuu Narendra Modi kuhusu uuzaji wa mazao yao.

Nchi hiyo pia, haikufunga mipaka yake wwala haikuzuia raia wa kigeni.

Hili linafaa kuwa funzo kwa nchi zingine ambazo zina mifumo dhaifu ya afya; kwamba kulegeza masharti na kupuuza ushauri wa wataalamu kuzuia msambao wa virusi hivi, kunaweza kuzua maafa makubwa kuliko hasara inayosababishwa na masharti hayo.

Kwa Kenya, ambayo hutegemea India kwa mahitaji ya dawa na matibabu, hali inaweza kuwa mbaya zaidi ikizingatiwa mfumo wetu wa afya ni dhaifu.

Ni nchi zinazokaza utekelezaji wa kanuni za afya na kuzidumisha, kuweka masharti makali na mikakati ya kulinda maisha ya raia wake – ikiwemo kuzuia raia wa kigeni wasio na shughuli muhimu – zinafaulu kukabiliana na janga hili.

Kila serikali inafaa kusisitizia raia wake kwamba corona imebadilisha mitindo ya maisha ya kijamii, kidini na kiuchumi.

Kuzingatia kanuni hizi kutawapa wanasayansi fursa ya kufuatilia mabadiliko ya virusi hivi na mbinu za kuviangamiza.

Kinachohitajika kwanza ni kuzingatia kanuni na masharti pasipo kuyalegeza kwa nia ya kutimiza maslahi ya watu wachache.

  • Tags

You can share this post!

Waamerika wafurahia utendakazi wa Biden siku 100 baadaye

WANDERI KAMAU: Buriani mhariri wetu mahiri Mauya Omauya