• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
WANGARI: Maslahi ya Wakenya wanaougua Ukimwi yasipuuzwe

WANGARI: Maslahi ya Wakenya wanaougua Ukimwi yasipuuzwe

Na MARY WANGARI

ENDAPO kuna watu ambao wamegubikwa na taharuki katika siku za hivi majuzi, basi ni Wakenya 1.5 milioni wanaougua ukimwi humu nchini.

Kuanzia uhaba wa dawa za kupunguza makali ya HIV (ARVs) zilizosababisha wahasiriwa kupunguziwa vipimo vyao vya kawaida, hadi ripoti za kushtua kuhusu kusambazwa kwa ARVs zenye sumu, ni dhahiri kuwa huu si wakati salama mno kwa wanaougua HIV.

Mapema mwezi jana, serikali ilivutia hisia kali kutokana na hatua yake ya kutaka kuanza kutoza kodi ufadhili wa dawa za ARVs kutoka shirika lisilo la kiserikali la USAID.

Mvutano huo ulisababisha uhaba wa ARVs ambapo wagonjwa wengi wangeweza kupata tu dawa za mwezi mmoja kinyume na kiwango kinachostahili cha dawa za miezi mitatu.

Wagonjwa wa Ukimwi tayari wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa kinga mwilini.

Kuwaongezea masaibu mengine kama vile kuwapunguzia ARVs, kuwataka kuwalazimu kununua dawa au kuwapa dawa zilizoharibika ni sawa na kuwaangamiza kabisa.

ARVs, sawa na bidhaa nyinginezo zinazoingizwa nchini kama msaada kutoka kwa mashirika ya kimataifa, hutozwa kodi.

Ni serikali tu kupitia Wizara ya Fedha inayoweza kuepusha bidhaa hizo dhidi ya kutozwa kodi kulingana na Sheria ya Awamu ya Tano kuhusu Usimamizi wa Kodi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akijibu ripoti kuhusu hatua ya kutoza kodi ARVs, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisisitiza kuwa serikali ni sharti ibuni mikakati ya kuwajali raia wake ili kuepuka matatizo sawia kujitokeza tena siku za usoni.

Sintofahamu

Licha ya hakikisho hilo, wagonjwa wa Ukimwi wangali wanaishi katika hali ya sintofahamu kuhusu mustakabali wao, huku hospitali nyingi za umma zikizidi kukabiliwa na uhaba wa ARVs kwa majuma kadhaa sasa.

Kina mama wajawazito wanaoishi na HIV wanakabiliwa na hatari ya kuwaambukiza watoto wao wachanga.

Uhalisia ni kuwa, Ajenda Kuu Nne kuhusu huduma bora kwa bei nafuu kupitia Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) kufikia 2030, ukiwemo mkataba wa dunia kuhusu HIV, zitasalia kuwa tu maandishi, iwapo hatua ya dharura haitachukuliwa.

Iwapo mamilioni ya Wakenya wanaougua HIV wataendelea kukosa dawa za kupunguza makali ya gonjwa hilo, basi itakuwa vigumu mno kufanikisha ajenda ya kimataifa kuhusu kuangamizwa kwa Ukimwi katika Bara la Afrika kufikia 2030.

Muhimu zaidi, serikali ni sharti iyape kipaumbele maslahi ya umma kwa kuwekeza katika miundomsingi thabiti ya kuimarisha raslimali za humu nchini ili kupunguza hali ya kutegemea ufadhili wa kigeni.

[email protected]

You can share this post!

ODONGO: Malumbano ODM ni ishara ya juhudi za kumrithi Odinga

Ushindani wa Marekani utadhuru maslahi ya nchi za Afrika,...