• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Wasanii wa Kayole kuzindua filamu mpya mwezi huu wa Julai

Wasanii wa Kayole kuzindua filamu mpya mwezi huu wa Julai

NA JOHN KIMWERE

WASANII wanaendelea kuungana ili kuzamia shughuli za kuzalisha filamu kwenye juhudi za kusaka mpenyo.

“Mwaka 2020 nilianzisha brandi iitwayo Eclab Records ambapo kwa sasa tuna wanachama 30 tunakolenga kufanya shughuli za kuzalisha filamu huku nia yetu ikiwa kufikia hadhi ya kimataifa,” mwenyekiti wake na produsa, Joseph Ondanga Onyango maarufu Joseph Chris amesema na kuongeza kuwa hakuna kisichowezekana.

Kundi hili tayari limezalisha filamu inayokwenda kwa jina ‘Dak Tek’ (Changamoto) iliyozinduliwa mapema mwaka huu 2022.

Kwa mara nyingine linajiandaa kuzindua filamu nyingine iitwayo ‘Malin’ Lin’g Mapondo’ (Neno Fiche).

Kundi hili limeundwa na wasanii wa Kayole ambao wamekuja na mpango huo kwenye juhudi za kutafuta riziki.

”Kiukweli mtaa wa Kayole una wasanii wengi tu waigizaji pia wanamuziki ambao wakishikwa mkono wanaweza kufanya makubwa na kutoa nafasi za ajira kwa wenzao wanaokuja,” akasema.

Uzinduzi huo utafanyika mwezi huu Julai,9, 2022, saa kumi na mbili jioni kwenye ukumbi wa Egesa Villa Umoja 1, Nairobi. Pia kwenye hafla kutakuwa na burudani ya muziki itakayotolewa na wanamuziki kadhaa akiwamo Emma Jalamo, Musa Jakadala, Dollar Kabari na Emily Nyaimbo wakiongozwa na MC Omondi Pengle.

Pia kando na masuala ya filamu brandi hii hurekodi fataki za injili pia nyimbo za mitindo mbali mbali za dunia ikiwamo Bongo, Ohangla na Gengetone kati ya nyinginezo.

Lebo hii imerekodi nyimbo za wanamuziki wanne kutoka Tanzania akiwamo Bussy F.

Kundi hili pia linajivunia kutoa filamu nyingine mbili ambazo ni ‘Chozi Langu’ na ‘Principal Man’.

“Katika mpango mzima tunalenga kuiga mfano wa kundi la Guardian Angel la filamu za Kinigeria (Nollywood),” anasema katibu wa Eclab Records, Stephen Odhiambo na kuongeza kuwa wana imani endapo watazamia mpango wao wamekaa vizuri kufanya makubwa ndani ya miaka mitano ijayo.

Pia anasema endapo wataendeleza ushirikiano wao vyema watafikia kiwango cha waigizaji mahiri nchini Nigeria kama Ramsey Noah na Mercy Johnson. Ramsey ameshiriki filamu kama ‘Weekend getaway,’ ‘The Millions,’ na ‘Nneka the Pretty,’ kati ya nyingine.

Naye Mercy Johnson anafahamika kwa filamu zake kama ‘Heart of a Fighter’, ‘The Maid’ na ‘Weeping Soul’ miongoni mwa nyingine.

”Wasanii ambao bado hatujapata mashiko tunastahili kufahamu kuwa uigizaji ni safari wala sio kuonekana kwenye runinga ni vyema kujiwekea msingi wa kuchuna hela siku zijazo,” katibu huyo akasema.

Anadokeza kuwa anaamini hatua ya kuunda kikundi cha uigizaji itasaidia kuinua sekta ya uigizaji nchini.

Anasema kuwa taifa hili limefurika wasanii wengi wanaume kwa wanawake lakini wamekosa ubunifu ili kuweka misingi thabiti kupaisha sekta ya uigizaji pia kuwasaidia kimaisha.

  • Tags

You can share this post!

Washirika wa Ruto na Kuria wazozana kuhusu kampeni

Viongozi wa Homa Bay wataka Raila awapelekee minofu katika...

T L