• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Washirika wa Ruto na Kuria wazozana kuhusu kampeni

Washirika wa Ruto na Kuria wazozana kuhusu kampeni

NA JAMES MURIMI

WASHIRIKA wa Naibu Rais na wa mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria wanaogombea viti mbalimbali kwa tiketi za vyama tanzu vya muungano wa Kenya Kwanza, kaunti ya Nyeri wanavutana kuhusu shinikizo za mfumo wa upigaji kura wa suti Agosti 9.

Spika wa Bunge la Kaunti ya John Kaguchia anashikilia kuwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kitaendelea kupigia debe wagombeaji wake pekee.

Bw Kaguchia, ambaye anawania kiti cha ubunge cha Mukurwe-ini kwa tiketi ya chama hicho, pia anasisitiza kuwa watamfanyia kampeni mgombeaji urais wa UDA William Ruto.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bw Kaguchia alisema kuwa UDA inaunga mkono upigaji kura kwa mfumo huo, maarufu kama “six piece” ili kuweza chama hicho kushinda viti vingi katika uchaguzi mkuu ujao.

“UDA ikishinda viti vingi, serikali ya Dkt Ruto itakuwa na nguvu kwani ajenda zake zitaweza kupitishwa kwa urahisi,” akaeleza.

Kulingana na Bw Kaguchia, viongozi wa vyama vingine tanzu katika muungano wa Kenya Kwanza pia wako huru kuwafanyia kampeni wagombeaji wa vyama vyao.

“Kwa mfano, hapa Nyeri kuna wagombeaji wa vyama vingine kama vile Chama Cha Kazi (CCK) kinachoongozwa na Bw Moses Kuria. Kwa kuwa yeye pia ni kinara ndani ya Kenya Kwanza, anafaa kuja kufanyia kampeni wagombeaji wa chama hicho,” Bw Kaguchia akaeleza.

Spika huyo alikariri kwamba UDA haitafanyia kampeni wagombeaji wa vyama vingine vilivyoko ndani ya muungano wa Kenya Kwanza.

“Tunawezaje kuwafanyia kampeni wagombeaji wengine wasiodhaminiwa na UDA ilhali tunashindana na wao? Waendeshe kampeni kivyao. Kila kinara anapaswa kuwafanyia kampeni wagombeaji wa vyama vyao,” Bw Kaguchia akasema.

Mipango yetu ni kuhakikisha kuwa viongozi katika kaunti ya Nyeri watachaguliwa kwa tiketi ya UDA na hii ndio sababu tunafanya kampeni kama timu moja,” akaongeza.

Spika Kaguchia alitoa kauli hizo baada ya baadhi ya wagombeaji wa viti mbalimbali katika kaunti ya Nyeri chini ya muungano wa Kenya Kwanza kupinga pendekezo wakazi wachague wagombeaji wa UDA pekee.

Walilalamika kuwa ni wagombeaji wa UDA pekee hupewa nafasi ya kuhutubu katika mikutano ya kampeni inayoongozwa na Dkt Ruto na mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua.

Bw Wachira Keen na Bw Peter Munyiri wanaowania kiti cha ubunge cha Kieni na kiti cha ugavana wa Nyeri mtawalia kwa tiketi ya CCK wanadai wao hutengwa wanapohudhuria mikutano ya kampeni ya Kenya Kwanza.

Bw Keen, ambaye ni mfanyabiashara, alitoa wito kwa Dkt Ruto kushughulikia suala hilo kwa haraka ili kuhakikisha kuwa wagombeaji wote wa vyama vya Kenya Kwanza wanatendewa haki.

“Sio haki kwamba tunapofanya mikutano ya pamoja, huwa hatupewi nafasi ya kuhutubu. Tunatoa wito kwa mgombeaji urais wa Kenya Kwanza kuhakikisha kuna usawa na wengine wasitengwe. Dkt Ruto akubali kila mtu,” akasema.

Bw Keen alisema kila mgombeaji anafaa kupewa nafasi kuhutubu katika mikutano ya Kenya Kwanza Nyeri na maeneo mengine ya Mlima Kenya.

“Sote tunamuunga mkono Dkt Ruto na ningependa kuwahakikishia kwamba Nyeri ni ngome yake. Tunataka kuendelea kumuunga mkono kama watu wa familia moja ili tushinde,” akaeleza.

Bw Munyiri alidai UDA haitaki kushirikiana na wagombeaji wengine wa vyama tanzu katika Kenya Kwanza, akionya hilo litamwathiri Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Ruto aapa kuandama Rais Kenyatta

Wasanii wa Kayole kuzindua filamu mpya mwezi huu wa Julai

T L