• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
ZARAA: Hawasubiri misaada tu, wao wanajikuzia chakula

ZARAA: Hawasubiri misaada tu, wao wanajikuzia chakula

NA LABAAN SHABAAN

MAKAO ya watoto ya Ruiru katika Kaunti ya Kiambu hayakai tu bure na kusubiri misaada kutoka kwa wahisani; inajisabilia na kujikuzia vyakula shambani kuzalisha matunda kama vile ndizi, parachichi, maembe na zambarau.

Yamkini wasimamizi wa kituo hiki cha watoto wanaamini kuwa, ukibebwa usilevyelevye miguu, kwa sababu kadhalika hukuza sukumawiki, spinachi, vitunguu, nyanya, miwa pamoja na kulea kuku na sungura kufikia utoshelevu wa chakula.

Mlezi wa Ruiru Rehabilitation Centre (RRC) Alfred Arega anasema hatua hii imewaokolea zaidi ya Sh50 000 kwa mwaka hivyo kusaidia kulipa karo ya shule kwa wanafunzi kadhaa.

“Moja ya mipango yetu ni kilimo ambacho kinahusisha watoto kama njia ya kuwashughulisha wakuze stadi za zaraa zaidi ya kujizalishia vyakula.” Arega anasimulia.

“Ni mradi muhimu katika kukuza ujuzi na maarifa yanayohitajika na mtaala wa umilisi na utendaji (CBC),” anaongeza.

Arega anaambia Akilimali kuwa mradi huu ulianza mwaka wa 2010 na kuwa baadhi ya watoto waliopitia hapa wanarejea kusaidia kukuza mradi zaidi.

“Vile vile, tumeanza mradi wa miche ya miti ya matunda ili kuuza na pia kupanda shambani humu. Waliofaidika kutokana na hifadhi hii ni wataalamu katika nyanja mbalimbali na wanatupiga jeki ili tujenge msingi wa kujisimamia,” Arega anaeleza.

RRC ina watoto 30 wanaojumuisha waliotelekezwa, mayatima na wengine wa wazazi wasiojiweza. Watoto hawa huenda katika shule za msingi na sekondari za kutwa karibu nao eneobunge la Ruiru huku wengine wakifaulu kusoma shule za bweni kupitia ufadhili.

Upepo wa kilimo hai umevuma pia katika miradi ya zaraa huku na umewasukuma wakulima hawa wachanga kujitengenezea mbolea kutoka kwa kinyesi cha mifugo na pia kutumia mabaki ya mimea shambani na sokoni.

“Tuliamua kufanya kilimo asili kuepuka magonjwa ya kimtindo kutokana na kemikali kwa sababu hatuna uwezo wa kutambua mboga asili kutoka sokoni na njia ya kipekee zaidi ni kujilimia mboga unayotaka,” Arega anaarifu.

“Si mboga tu. Pia tumeanza kukuza miche ya miti ya matunda kupitia upandikizaji. Mbali na kupata fedha na matunda tunafuata mkondo wa nchi kupanda miti kukabili matatizo ya mazingira yanayokuja na mabadiliko ya tabianchi,” anaongeza.

Mlezi wa watoto hawa hupanga ratiba ya kazi ya watoto shambani wakati hawako shuleni hususan asubuhi, jioni na wikiendi. Watoto hawa huongozwa na wafanyakazi walioajiriwa kituoni humu.

Wanalenga kujitosheleza siku za usoni kwa kukaza kamba zaidi kuzalisha chakula cha matumizi na cha kuuza ili kukidhi ada za maji, umeme, karo na nyinginezo.

Joseph Mutunga abeba sukuma wiki aliyovuna shambani katika hifadhi ya watoto Ruiru. PICHA | LABAAN SHABAAN

RRC iko katika shamba la ekari tatu ambapo ekari moja hutumika kwa kilimo na nyingine zikitumika kwa makazi na uga wa michezo.

Arega anasema japo wanategemea hisani kutoka kwa wasamaria wema, juhudi zao bado zinahitaji msaada zaidi kufanikisha mradi wa kilimo hasaa kupata pembejeo.

“Tukipata shirika la kutufaa na miche ya miti ya matunda, wilbaro, majembe, panga, mbolea na vifaa vingine tutajitegemea kuliko kungoja misaada,” Arega anaomba wahisani wawasaidie kuimarisha mradi wao wa kilimo.

Kituo cha Kuhifadhi Watoto cha Ruiru kinaamini kuwashughulisha watoto katika kilimo na shughuli nyingine huwaondolea kiwewe na kuwanawirisha kisaikolojia wasahau matatizo ya maisha yao na kukua kikamilifu katika nyanja mbalimbali za maisha.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya kushiriki Jumuiya ya Madola ya chipukizi Trinidad...

Dereva Maxine Wahome akana kumuua mpenzi wake na dereva...

T L