• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 9:55 AM
ZARAA: Kilimo endelevu chamfaa nyanjani na kuinua mapato

ZARAA: Kilimo endelevu chamfaa nyanjani na kuinua mapato

NA SAMMY WAWERU

CATHERINE Mbili amekuwa mkulima wa nafaka kwa zaidi ya miaka 25 Kaunti ya Makueni, eneo ambalo ni kame.

Aliingilia kilimo kama njia mojawapo ya kukidhi mahitaji ya familia yake kupitia mazao ya mahindi na maharagwe.

Ikiwa shughuli ambayo haikuwa ikimuingizia faida, anasema ilikuwa vigumu kuipanua.

Mwaka 2015, miaka 20 baadaye aligeuza jitihada zake kuwa kilimobiashara, kupitia utangamano na Shirika la Chakula na Kilimo la Muungano wa Umoja wa Mataifa (FAO) na taasisi ya The International Crops Research Institute for Semi-Arid Tropics (ICRISAT).

Kulingana na Catherine, kupitia kikundi cha wanachama 15 walichoanzisha, walijuzwa kilimo cha nafaka zinazostahimili makali ya ukame, kama; pojo, mtama, mbaazi, kunde, mawele na wimbi.

Pia hukuza mchicha (terere) ili kupata mbegu. Kundi hilo la kina mama, Twone Mbee Mukolekya, kufikia sasa lina idadi jumla ya wanachama 25.

“ICRISAT ilitufunza kuhusu nafaka zinazohimili athari za ukame, na kutupa mbegu za kutanguliza,” asema. Ni kupitia hamasisho la shirika hilo, walipevushwa ushirikiano kama wanachama kuchanga fedha kununua mbegu bora na zilizoimarishwa.

“Isitoshe, tulinufaika kupata mafunzo ya kilimo endelevu na hifadhi, na zaidi ya yote kutafutia mazao soko,” mkulima huyo aelezea.

Kilichompiga jeki zaidi ni uongezaji thamani.

Catherine Mbili, akielezea Mkurugenzi Mkuu ICRISAT, Dkt Jacqueline Hughes (aliyevalia miwani) bidhaa anazoongeza thamani kwa kutumia unga wa nafaka. PICHA | SAMMY WAWERU

Unga wa nafaka anazolima kwenye ekari tatu, Catherine anautumia kuoka keki za harusi, keki ndogo, biskuti, mandazi, chapati na ugali. Hali kadhalika, mama huyu hupika uji, pilau ya mtama na mkate.

Anasema kuwa vifaa vingi anavyotumia ni vile vinavyotumika jikoni. “Nilichokosa ni mashine ya kuoka keki na mkate pekee, hutegemea ya mkulima mwenza,” asema.

“Nikiipata nitakuwa na kiwanda kamilifu,” anaongeza.

Baadhi ya vitu anavyotumia kuongeza thamani ni mafuta ya kupikia, siagi, mayai, ndimu, unga wa ngano, maziwa, chumvi na sukari, akisisitiza bidhaa zilizosindikwa zina mapato ya haraka.

Soko lake likiwa rejareja, andazi huuza Sh10, keki moja ndogo haipungui Sh30 na za harusi na hafla, hulingana na maelewano na mteja.

Kilimo ni nguzo kuu ya ukuaji wa uchumi na maendeleo nchini, ila kinatatizwa na athari za tabianchi.

Misimu ya mvua isiyotabirika na kiangazi na ukame wa mara kwa mara, asilimia 95 ya mimea ikitegemea mvua kunawiri.

“Ni muhimu kuhamasisha wakulima na kuwasaidia kukumbatia mimea inayostahimili kero ya tabianchi. Muhimu zaidi, wahimizwe kuongeza mazao thamani ili kuteka soko bora,” asema Dkt Jacqueline Hughes, Mkurugenzi Mkuu ICRISAT, akiahidi shirika hilo kuendelea kuinia wakulima nchini hasa katika maeneo kame.

Catherine, alikuwa miongoni mwa wakulima waliotambuliwa na shirika hilo mwaka huu wakati likiadhimisha miaka 50 katika utendakazi wake. Akiwa na uzoefu wa miaka mingi kwenye zaraa, mama huyo hufunza wakulima wenza mifumo ya kilimo endelevu na uongezeaji thamani.

You can share this post!

Vijana wanawiri licha ya kukosa umahiri wa lugha

Sababu ya Muturi kuahirisha kikao maalum

T L