• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Sababu ya Muturi kuahirisha kikao maalum

Sababu ya Muturi kuahirisha kikao maalum

NA CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amefutilia mbali kikao maalum ambacho kiliratibiwa kufanyika leo Jumatano, Julai 13.

Kwenye taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari Jumanne, Julai 12, Bw Muturi alisema alichukua hatua hiyo baada ya serikali kudinda kuchapisha notisi ya kuitisha kikao hicho katika gazeti rasmi la serikali.

Kisheria, notisi ya kutoka kwa Spika wa Bunge la Kitaifa au Spika wa Seneti ya kuitisha kikao maalum cha mabunge hayo sharti ichapishwe katika gazeti rasmi la serikali ili iweze kuwa halali.

“Kutokana na hali hiyo, nawaarifu kuwa vikao maalum vya bunge la kitaifa ambavyo viliratibiwa kufanyika kesho, Jumatano, Julai 13, 2022 vimefutiliwa mbali.

“Nawaomba radhi wabunge kwa usumbufu wowote ambao umesababishwa na kufutiliwa huko kwa vikao hivyo,” Muturi akasema.

Spika huyo alisema Mchapishaji Mkuu wa serikali alikataa na kufeli kuchapisha notisi ya vikao hivyo ambavyo vingefanyika asubuhi na alasiri “bila kutoa sababu iliyochangia hatua hiyo.”

“Hii ni licha ya kwamba stakabadhi zote ziliwasilishwa kwa afisi yake kwa wakati wiki jana,” Muturi akaeleza.

Spika huyo aliitisha vikao hivyo maalum kutoa nafasi kwa wabunge kujadili Mswada wa Kutenga Fedha zaidi kwa Serikali za Kaunti na Mswada wa Huduma Namba, 2021, ambao ulizua utata.

Aidha, wabunge walitarajiwa kutumia muda huo kuidhinisha Makubaliano wa Mwafaka wa Ushirikiano kati ya Idara za Ulinzi za Kenya na Uingereza pamoja na Ireland Kaskazini.

Wandani wa Naibu Rais William Ruto wamepinga sehemu fulani za Mswada wa Huduma Namba, 2021 ambao inalenga kuweka mwongozo wa kisheria wa kuwezesha usajili wa watu kidijitali katika mfumo wa KIEMs.

Awali, wabunge wanaoegemea muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya walikuwa wameapa kutohudhuria kikao hicho maalum.

Wakiongozwa na kiongozi wa wachache John Mbadi na kiranja wa wachache Junet Mohamed walisema mkutano huo uliitishwa bila notisi hiyo kuchapishwa katika gazeti rasmi la serikali.

Bunge la kitaifa lilikuwa limeahirisha vikao vyake Juni 9, 2022 bila kuweka tarehe ya kujea, ili kutoa nafasi kwa wabunge kuendesha kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Kilimo endelevu chamfaa nyanjani na kuinua mapato

UJASIRIAMALI: Bidhaa zake zavutia wateja tele ughaibuni

T L