• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
ZARAA: Mikakati ya kufufua kahawa sasa yaanza kuzaa matunda

ZARAA: Mikakati ya kufufua kahawa sasa yaanza kuzaa matunda

NA SAMMY WAWERU

GLADYS Wangu na mume wake, Christopher Wambugu wamekuwa katika kilimo cha kahawa kwa zaidi ya miaka 15.

Wakiendeleza ukulima huo eneo la Mathira, Nyeri, ikiwa kuna mwaka malipo yamekuwa ya kuridhisha wanataja ni 2022.

Ni malipo ya mazao waliyovuna mwaka 2021. Kwa desturi, kahawa hulipwa mwaka mmoja baada ya mavuno kupitia mashirika na kampuni zinazoyatafutia soko ndani na nje ya nchi.

“Kipindi cha muda ambao tumekuwa tukilima kahawa, malipo ya mwaka huu yamekuwa bora zaidi. Kila kilo tumelipwa Sh109,” Wangu adokeza.

Huuza mazao kupitia kiwanda cha Karie, ambacho ni mwanachama wa Rutuma Amalgamated Farmers Co-operative Society.

Kulingana na Wangu, kabla ya kuanza kuboresha mikahawa yake miaka mitatu iliyopita, kilo moja ilikuwa ikichezea kati ya Sh50 – 70. Akiitaja kuwa duni anasema iliwashinikiza kupuuza kuishughulikia.

“Kukidhi karo ya watoto wetu ilikuwa kibarua,” asema mama huyo wa watoto wawili.

“Malipo ya sasa, yametuwezesha kusomesha wajukuu,” aelezea.

Wanandoa hao wana jumla ya mikahawa 220, aina ya Ruiru 11.

Simulizi yao si tofauti na ya David Karira.

David Karira ambaye ni mkulima wa kahawa katika Kaunti ya Nyeri. PICHA | SAMMY WAWERU

Naye alianza kuboresha mikahawa yake 350 miaka mitano iliyopita.

“Miaka iliyotangulia, niliachilia mimea yangu kwa sababu ya malipo duni,” Karira asema.

“Awali, nilikuwa na kahawa aina ya SL niliyoiimarisha kwa kupandikiza na ya Ruiru 11,” aelezea.

Dalili za soko kunoga zilimchochea. Karira pia huuza mazao yake kupitia kiwanda cha Karie, na anaambia Akilimali mwaka 2021 alivuna zaidi ya kilo 2,000.

Wangu anafichua alivuna kilo 1,200.

Malipo waliyopata wanayaridhia, wakipongeza serikali kwa jitihada zake.

Timothy Mirugi, Meneja Mkuu New KPCU – Taasisi ya serikali iliyo na jukumu la kutafutia wakulima soko, anasema tabasamu ya wakulima 2022 inatokana na mikakati ya serikali kuimarisha sekta ya kahawa.

Mwaka 2019, Rais Uhuru Kenyatta alifanya mabadiliko katika KPCU ya kitambo.

Mkulima anahusishwa katika hatua zote za mazao yake; kuyapima na kujua kilo zilizosagwa, kisha anakabidhiwa bili. Kulingana na Mirugi, hatua hiyo imesaidia kukabili vilivyo wizi wa mazao.

“Isitoshe, kubuniwa upya kwa New KPCU kumeleta ushindani mkuu miongoni mwa kampuni na mashirika yanayosaka wanunuzi,” afisa huyo afafanua.

Taasisi hiyo inaendelea kuandikisha wakulima wapya, ikiwa na mabohari maeneo yanayokuza kahawa nchini.

“Mazao yanapofika mikononi mwetu, ni salama. Tumeimarisha ulinzi.”

Kupitia programu za kufufua sekta ya kahawa Kenya, serikali inasambazia wakulima fatalaiza ya bei nafuu.

Mfuko wa kilo 50 ukiuzwa zaidi ya Sh6, 000, wakulima wa kahawa kupitia vyama vyao vya ushirika kiwango hicho wanakipata na kati ya Sh3, 100 – 3, 600. Zaidi ya wakulima 70, 000 wamenufaika.

“Wanagharimia asilimia 60, na serikali asilimia 40,” afisa huyo adokeza.

Mkakati huo pia unajumuisha dawa za magonjwa na wadudu.

Mirugi anasema serikali imetoa mkopo wa Sh2.7 bilioni kupiga jeki wakulima, wa riba ya chini.

Kufikia sasa, mkopo huo maarufu kama cherry funds, zaidi ya Sh200 milioni zimesambazwa, ukilenga wakulima wote wa kahawa.

Ni mikakati inayotia wakuzaji motisha, Wangu na Karira wakiifurahia japo wanahimiza serikali kuwaboreshea soko angaa kilo moja kugonga Sh200.

Mirugi anasema mazuri yaja, bei ya mwaka huu akihoji ilikuwa kionjo tu. Ujerumani, Marekani na Korea Kusini ndio wateja wakuu wa kahawa ya Kenya.

  • Tags

You can share this post!

NJENJE: Mapato ya uuzaji mboga na matunda yashuka,...

Raila sasa akimbilia mahakama

T L