• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 7:52 PM
NJENJE: Mapato ya uuzaji mboga na matunda yashuka, uzalishaji ukipungua

NJENJE: Mapato ya uuzaji mboga na matunda yashuka, uzalishaji ukipungua

NA WANDERI KAMAU

MAPATO ya uuzaji wa mazao ya kibiashara nchini yalishuka kwa Sh32 bilioni katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, zimeonyesha takwimu.

Mazao hayo yanajumuisha maua, mboga na matunda.

Kulingana na Idara ya Kusimamia Uuzaji wa Mazao hayo (HDK), mapato ya uuzaji wa mazao hayo yalipungua kwa asilimia 40—kutoka Sh80.7 bilioni hadi Sh48.4 bilioni wakati sawa mwaka 2021.

Idara hiyo ilisema kuwa hali hiyo ilisababishwa na kupungua kwa uzalishaji wa mazao hayo na kupungua kwa maparachichi ya kiwango cha juu, kama inavyohitajika na masoko kutoka nje.

Parachichi nyingi zilizosafirishwa nje ya nchi hazikuwa zimekomaa ifaavyo. Ripoti zilieleza kuwa parachichi nyingi zilikataliwa, hali ambayo imewalazimu wadau katika sekta hiyo kuanza kutekeleza mikakati mipya.

“Mauzo yetu yalishuka pakubwa, hali iliyoathiri mapato yetu kwa jumla. Vile vile, parachichi zetu zilikuwa na matatizo kwenye ubora wake,” ikasema idara hiyo.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa kiwango cha matunda kilishuka kutoka kilo 82.1 milioni hadi kilo 44 milioni.

Idara hiyo ilikuwa imetabiri kuwa mapato ya uuzaji wa mazao hayo yangeongezeka kutoka mwezi Aprili kwenda juu, baada ya mataifa kama China kuondoa marufuku dhidi ya uuzaji wa parachichi kutoka Kenya.

Hata hivyo, Kenya bado haijaanza kupata mafanikio ya kuondolewa kwa marufuku hiyo.

Mapato kutoka uuzaji wa maua yalipungua kutoka Sh53.2 bilioni mwaka uliopita hadi Sh37.3 mwaka huu.

Mapato ya uuzaji matunda yalishuka kutoka Sh12 bilioni mwaka uliopita hadi Sh5.6 bilioni mwaka huu, huku mapato ya uuzaji mboga yakishuka kutoka Sh10.1 bilioni hadi Sh5.4 bilioni.

Maua huwa yanajumuisha kiwango cha juu zaidi cha mazao ya kibiashara yanayouzwa na Kenya mataifa ya nje.

Mwaka 2021, Kenya ilipata mapato ya kihistoria—Sh158 bilioni—kutokana na uuzaji wa mazao hayo.

Mazao hayo ndiyo yameizalishia Kenya mapato ya juu zaidi ya fedha za kigeni kwa miaka miwili iliyopita, ikilinganishwa na sekta ya majanichai na utalii.

Mataifa ya Ulaya bado yanaendelea kuongoza kwa kuwa soko bora kwa mazao hayo kutoka Kenya.

You can share this post!

Kenya Kwanza kufanya mkutano wa kwanza

ZARAA: Mikakati ya kufufua kahawa sasa yaanza kuzaa matunda

T L