• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
BENSON MATHEKA: Ruto anafanya vyema kuzuru ngome za Upinzani, bora tu apunguze siasa

BENSON MATHEKA: Ruto anafanya vyema kuzuru ngome za Upinzani, bora tu apunguze siasa

NA BENSON MATHEKA

RAIS William Ruto amefanya kile ambacho kiongozi wa nchi anafaa kufanya; kuunganisha taifa. Amekuwa akitembelea kaunti zinazochukuliwa kuwa ngome za upinzani na kuahidi au kuanzisha miradi ya maendeleo.

Hisia za wafuasi wake zinaonyesha kuwa wangefurahi kama angeanza kwa kutembelea ngome zake na kuwapa ‘minofu’ kama njia moja ya kuwashukuru kwa kumpigia kura kwa wingi katika uchaguzi mkuu uliopita.

Lakini akiwa kiongozi wa nchi, Katiba aliyoapa kulinda na kutetea inamtaka kuwa nembo ya utaifa, kumaanisha ni Rais wa Wakenya wote popote walipo na anastahili kuwakilisha maslahi yao nje ya nchi.

Kufikia sasa, Rais Ruto amefanya hivyo na hivyo basi, amefaulu kuzima vigogo wa upinzani ambao wangetumia hali ya kutengwa kwa ngome zao kumlaumu.

Ametembelea kaunti za Homa Bay (mara mbili), Siaya, Machakos, Kitui, Mombasa (mara mbili) na Turkana ambako amekutana na wakazi na viongozi na kuwahakikishia kuwa serikali yake haitabagua sehemu yoyote kwa msingi wa kikabila na kisiasa.

Amekutana na magavana wa Kisumu, Kakamega, Kisii na Vihiga kujadili miradi na ushirikiano.

Japo kuna wanaomlaumu kwa kukumbusha wakazi wa ngome za upinzani kwamba hawakumpigia kura kwa wingi, anakuwa mkweli kwa kusema hivyo. Yeye ni mwanasiasa na kazi yake ni siasa, bora isifunike jukumu lake kama kiongozi wa nchi.

Yamkini anafaa kuzingatia maoni ya wakazi wa maeneo anayotembelea kuhusu miradi wanayotaka ipewe umuhimu, na muhimu zaidi, kuhusu nafasi serikalini kwa kuwa ukweli ni kwamba kuna ukosefu wa usawa katika uteuzi wa nyadhifa kuu serikalini.

Hapa, Rais Ruto anahitaji kuchukua hatua kuimarisha utaifa katika serikali inavyosema Katiba.

Amejaribu kuteua watu kutoka ngome za upinzani katika serikali yake lakini, kusema ukweli na ukweli anaopenda, kuna maeneo na jamii zinahisi kupuuzwa katika suala hili.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Mbinu za kuteua wanafunzi wa Kidato cha 1...

Hisia mseto polisi sasa wakinyoa wenye rasta

T L