• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Hisia mseto polisi sasa wakinyoa wenye rasta

Hisia mseto polisi sasa wakinyoa wenye rasta

NA MWANGI MUIRURI

SHERIA mpya ambayo haijarekodiwa na inayotekelezwa na maafisa wa polisi katika baadhi ya maeneo ya Murang’a Kusini imeifanya kuwa marufuku kwa wanaume kufuga nywele na kuzisuka kwa mtindo wa rasta.

Maafisa wa polisi wanawasaka wanaume na kuwalazimisha kunyoa huku wanawake wakiruhusiwa kufuga na kusuka nywele kwa mtindo huo bila vikwazo.

Hatua hiyo imeibua hisia mseto miongoni mwa wakazi wa Murang’a Kusini huku baadhi wakiipinga na wengine wakiishabikia.

Wakazi wanatania jambo hilo ambalo yamkini linaashiria kurejea kwa enzi za aliyekuwa msimamizi wa eneo hilo, marehemu Bw Fred Mwango ambaye aliwalazimisha wadogo wake kunyoa nywele za rasta katika miaka ya 1980.

Wadi ya Kamahuha ni moja kati ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi. Takriban barobaro 56 wamelazimishwa kunyoa nywele zao za rasta katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

“Acha wavulana hawa waonekane watanashati…watakana haya, lakini tunajua wale wanafuga rasta wanavuta na kuuza bangi, wanaiba na ni mfano mbaya kwa watoto wetu,” alisema Bi Martha Njeru, mfanyabiashara katika soko la Kamahuha.

Yamkini ni mpango wa maafisa wa ulinzi eneo hilo ikizingatiwa kuwa doria zinazopigwa na polisi zinalenga tu kuwatia mbaroni wenye rasta.

“Tusifanye jambo hili kuwa suala kubwa..polisi wanajua ni kwa nini wanalazimisha watu hawa kunyoa rasta. Baadhi huzifuga tu kama kitambulisho cha ukaidi…vijana ambao ni waasi hufikiri rasta huwafanya kuogopwa,” alisema James Kiama ambaye ni kiongozi wa vijana mjini Sabasaba.

Alisema mojawapo ya hatia mbaya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya eneo hilo ilitekelezwa na vijana waliofuga rasta.

“Ni katika eneo hili ambapo vijana walikamatwa mnamo 2013 kwa kujamiiana na punda…walifunga mnyama huyo karibu na uwanja wa kanisa na wakaendelea kufanya kitendo hicho cha kinyama na baadaye wakaua punda huyo. Walikuwa na rasta,” alisema mkazi kwa jina Martin Munene.

Aidha, ni katika eneo hilo ambapo kaka wawili waliofuga rasta wanashukiwa kumbaka na kumuua mama yao ndani ya boma alikoolewa mnamo Februari 5, 2022. Wawili hao wanajitetea mbele ya korti.

Mjadala kuhusu suala hilo ambalo limeibua wasiwasi kuhusu hali ya usalama limegeuka mzaha huku wanawake wakiwa idadi kubwa ya wanaounga mkono unyoaji huo.

“Baadhi ya vijana hawa watakufa kutokana na utapiamlo ikiwa hawataokolewa na polisi kunyoa rasta zao. Nywele za rasta hufyonza madini tele kutoka mwilini na ndiyo sababu wanaozifuga nywele hizo za rasta huonekana waliodhoofika kiafya,” alisema Bi Esther Ndirangu, mfanyabiashara katika kijiji cha Kamuiru.

Aliongeza kuwa mitindo ya rasta inahitaji kufugwa na watu walio safi, wanaojua kuoga.

“Baadhi ya wavulana hawa wana nywele za rasta zinazofanana na vichaka vidogo vichafu. Serikali inafanya vyema kuwafanya waonekane nadhifu. Ninaweza kuchangia kuwezesha wengi iwezekanavyo wanyolewe nywele hizo,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Ruto anafanya vyema kuzuru ngome za...

Watu 600,000 wameuawa katika vita Tigray – Obasanjo

T L