• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
CHARLES WASONGA: Uhuru na Mohamud wasuluhishe zogo la mpaka wa Bahari Hindi kabla ya Agosti 9

CHARLES WASONGA: Uhuru na Mohamud wasuluhishe zogo la mpaka wa Bahari Hindi kabla ya Agosti 9

NA CHARLES WASONGA

HATUA ya Somalia kuruhusu tena uuzaji wa miraa ya Kenya nchini humo na safari za ndege za shirika la Kenya Airways (KQ) kati ya Nairobi na Mogadishu ni habari njema kwa wakulima na wafanyabiashara wa zao hilo.

Aidha, hatua hiyo inatarajiwa kurejesha uhusiano mzuri kati ya Kenya na taifa hilo jirani; uliokuwa umezorota.

Kwenye taarifa iliyotolewa baada ya mkutano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Rais mpya wa Somalia, Bw Hassan Sheikh Mohamud jijini Nairobi wiki jana, nchi hizi mbili pia zitashirikiana katika vita dhidi ya ugaidi.

Rais Kenyatta pia aliamuru kufunguliwa kwa mpaka wa Kenya na Somalia ili kufufua biashara kati ya mataifa hayo mawili.

Mpaka huo ulifungwa mnamo 2019, kufuatia ongezeko la mashambulio ya kigaidi nchini, yaliyoaminika kutekelezwa na wanachama wa Al Shabaab kutoka Somalia.

Lakini maafisa wa usalama wa mataifa haya mawili wanafaa kuwa macho magaidi wasije wakatumia nafasi hiyo kuendeleza mashambulio. Maafisa wa usalama wa nchi hizi mbili pia wanapaswa kuwaandama raia wao ambao huwasaidia wapiganaji hao kuendesha maafa.

Vile vile, Rais Kenyatta anayeondoka mamlakani baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, anafaa kutoa maelezo kuhusu hatima ya mzozo kati ya Kenya na Somalia kuhusu eneo fulani la mpakani katika Bahari Hindi.

Oktoba 2021, majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), iliyo jijini The Hague, Uholanzi, waliamua kuwa sehemu kubwa ya eneo hilo iko ndani ya Somalia.

Lakini Rais Kenyatta alisema Kenya haitaheshimu uamuzi huo akishikilia kuwa sehemu hiyo, yenye utajiri mkubwa wa mafuta, gesi na samaki, iko katika himaya ya Kenya.

Lakini katika mkutano huo wa majuzi kati ya marais hao wawili, mzozo wa mpaka wa bahari Hindi haukuzungumziwa. Marais hao wawili wanafaa kutatua mzozo huo, kabla ya Rais Kenyatta kuondoka mamlakani.

  • Tags

You can share this post!

Raha tele mwanariadha Kasyoka akimtunuku baiskeli daktari...

CECIL ODONGO: Ruto acheze kizalendo asije akatumbukiza...

T L