• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:50 AM
DOUGLAS MUTUA: Kulazimishia Waafrika ushoga hakika ni ukoloni mamboleo

DOUGLAS MUTUA: Kulazimishia Waafrika ushoga hakika ni ukoloni mamboleo

USASA una matatizo.

Na kuukimbiza usasa humwacha mtu katika hali ya kukanganyikiwa asitofautishe kushoto na kulia, ukweli na uongo.

Ilivyo hulka ya binadamu, hasa akiwa maarufu, huwana kuonekana mja wa kisasa kwa vyovyote vile ili akubalike na jamii ya kisasa, kwa imani eti akikubalika atakuwa amekamilika.

Kiongozi wa kanisa Katoliki kote duniani, Papa Francis, katika jaribio la kuufikia usasa, na labda kukubalika na mataifa ya kimagharibi, amejipata kwenye njia-panda ya kisitankisia.

Sasa anatufafanulia tofauti kati ya dhambi na uhalifu kana kwamba hatujui, ili kujaribu kutueleza kwa nini ushoga umekuwa ukitakaswa na makao makuu ya Katoliki tangu achukue usukani wa kanisa hilo.

Rais wa 44 wa marekani, Barrack Obama, alipotaka kuchaguliwa kwa kipindi cha pili, alidai kwamba keshapevuka na kulielewa suala hilo nyeti la ngono kati ya watu wa jinsia moja.

Kama Papa Francis, Bw Obama alitamani sana kukubalika na mrengo wa kisiasa wa Marekani unaoutukuza ushoga na kulazimisha kila mtu aukubali bila kuuliza maswali ya kimsingi.

Papa Fancis alizaliwa Argentina, naye Bw Obama, japo kazaliwa Marekani, ana asili ya Kenya, hivyo utamaduni wa Marekani na mataifa ya magharibi yanayoeneza ushoga si wao.

Na hilo wanalifahamu fika, hivyo katika juhudi zao za kujitiatia ili wakubalike kama wamoja kundini, wanafanya maamuzi ya ajabu na kujiingiza katika mijadala isiyo na tija kamwe.

Mathalan, tunajua na tunatambua kwamba Marekani na mataifa mengi ya magharibi wa Uropa yana sheria zinazowalinda mashoga kwa jumla. Tunaheshimu sheria hizo, hivyo hatuwezi kumbagua wala kumshambulia mtu kwa misingi ya tabia hiyo iliyo kinyume na maumbile. Sheria ni kubwa kuliko alioyeitunga.

Hata hivyo, kwa kuwa nasi tuna haki za kujieleza na kuabudu, tunadai kuheshimiwa na kuachwa tuseme ya nyoyoni pasi na kuzuiwa kwa kuwa huu ni ulimwengu huru.

Binafsi nimekerwa na matamshi ya Papa Francis kwa sababu ameyatoa siku chache kabla ya kuanza ziara yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Sudan Kusini.

Papa anaudhi kupindukia, hasa ikizingatiwa kwamba Afrika kuna wanaume wengi waliolawitiwa na mapadre wa Katoliki na Papa Francis hajafanya chochote kuwatendea haki.

Afrika, kando na kwamba tamaduni zetu haziruhusu ushoga, tuna mambo mengi muhimu ya kuwazia, na ngono si miongoni mwayo. Mioyo na bongo zetu zipo tayari kuhubiriwa neno la Mungu, si kupawa lishe ya siasa duni za kujamiiana kwa jinsi ambayo hata wanyama hawajaribishi!

Walio na kila kitu maishani wanaweza kutumia muda wao wa burudani wakijadili ngono, ya kawaida au ya kinyume na maumbile, kwa kuwa kwao matatizo ya kiuchumi si hoja.

Na msimamo wetu huo unapaswa kuheshimiwa, si kubezwa hata kidogo! Hatupanii kukubalika na yeyote, wala hatuukimbilii usasa kama unavyoeleweka na wageni.

Kabla ya kuzuru Afrika katikati ya wiki hii, Papa Francis anapaswa kumpigia simu Bw Obama amuulize jawabu alizopata alipojaribu kueneza ‘injili’ ya ushoga barani Afrika.

Kimsingi, Ikiwa Afrika imekataa ushoga, kujaribu kuilazilimshia ni ukoloni mambo-leo na jaribio la kutunyanyasa tena linapaswa kupingwa na kila aliye na akili razini.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

KASHESHE: Elba aipa shavu KE

Mamake Koigi wa Wamwere kufidiwa Sh2.5 milioni

T L