• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
KINYUA KING’ORI: Ni haki ya kila Mkenya popote kupelekewa maendeleo bila ubaguzi

KINYUA KING’ORI: Ni haki ya kila Mkenya popote kupelekewa maendeleo bila ubaguzi

HATUA ya Rais Dkt William Ruto kuzuru Nyanza hivi majuzi na kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo huku akiahidi kufufua yote iliyokwama eneo hilo na kote nchini, instahili kupongezwa.

Hatua hiyo itachangia mno kukuza utangamano nchini maana wananchi wa maeneo hayo kwa miaka mingi hutengwa katika mipango ya maendeleo, kwa kuonewa au kupuuzwa kutokana na misimamo yao kisiasa.

Kiasi cha wao kujihisi hawana haki na usawa katika nchi yao, na kuendelea na siasa kali za upinzani.

Juhudi za Rais kuamua kutekeleza majukumu yake bila ubaguzi kwa kuhakikisha kila eneo nchini linanufaika na miradi ya serikali ya kitaifa, zitazaa matunda haswa katika maeneo yanayoaminika kuwa ngome za upinzani.

Katika hotuba zake Ruto amekariri kujitolea kwake na serikali ya Kenya kwanza kuunganisha taifa, kwa kuhakikisha Wakenya wote wanatendewa haki bila hujuma au bezo za kisiasa.

Madhumuni yake ni kukoleza umoja, amani na usalama na kupunguza joto la kisiasa pamoja na maonevu ya kikabila yanayoshuhudiwa kila baada ya uchaguzi mkuu.

Serikali ya kitaifa ikisimama kidete kutumia raslimali zake vizuri kuona raia wanapewa mandhari bora kuendeshea shughuli zao za ujenzi wa taifa, watakumbatia serikali na hata kujivunia taifa lao.

Kunusuru taifa lililogawanyika kisiasa kama Kenya, Rais anafaa kuwa kioo cha umoja wa taifa kwa kusambaza maendeleo kote na kustawisha maisha ya raia wote bila ubaguzi au mipaka ya kisiasa.

Ni hatua kama hizo zinaweza kuwapa tabasamu hata wafuasi wa mrengo wa upinzani, Azimio, na kuwashawishi kushirikiana na serikali kwa hiari yao.

Hivyo, miradi iliyoanzishwa na Rais kule Homa Bay na Siaya haitoshi; kuna umuhimu wa kuisambaza maeneo mengine kama vile Pwani, Magharibi hadi Kaskazini Mashariki ili kuleta ssawa wa maendeleo.

  • Tags

You can share this post!

MAGWIJI WA WIKI: The Munenes

Familia kuzika jeneza bila maiti kutimiza desturi

T L