• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Familia kuzika jeneza bila maiti kutimiza desturi

Familia kuzika jeneza bila maiti kutimiza desturi

NA DERICK LUVEGA

FAMILIA moja katika Kaunti ya Vihiga, imekasirishwa na uamuzi wa mwili wa jamaa yao aliyefariki akiwa ng’ambo kuchomwa, na sasa inapanga mazishi mwigo ambapo watazika jeneza bila maiti.

Mzee Daniel Etisi, 82, alifariki akiwa New Jersey, Amerika Novemba 30, 2022, na mwili wake ukachomwa kulingana na mapenzi yake.

Lakini familia yake katika kijiji cha Ebulonga, Emuhaya, Kaunti ya Vihiga, haikufurahishwa na uamuzi huo na inasisitiza lazima ifanye mazishi yake hata bila mwili.

Familia hiyo inapanga kufanya mazishi mwigo ambayo itazika jeneza likiwa na majivu ya mwili wake uliochomwa. Mazishi hayo yatahusisha desturi zote za mazishi zinazofanywa mwili ukiwemo.

Mjane wa marehemu, Bi Grace Amiana, anasema kwamba mazishi hayo sasa yatafanywa Januari 20, baada ya majivu kuwasili nchini Januari 9, zaidi ya mwezi mmoja tangu mumewe alipofariki.

Hata hivyo, alisema, waombolezaji hawataruhusiwa kutazama majivu hayo.

Mazishi hayo ambayo ni ya kwanza ya aina yake kaunti ya Vihiga, ni ujumbe kwamba family nyingi za kiafrika, hazijakumbatia uchomaji wa maiti.

Bi Amiana alichukua majivu hayo kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kisumu mnamo Januari 11. Alisema kwamba majivu hayo yatawekwa ndani ya jeneza siku ya mazishi na picha ya marehemu mumewe kuwekwa juu yake ili waombolezaji watazame.

Bi Amiana alisema hakukubaliana na mumewe alipomfahamisha alitaka mwili wake uchomwe akifariki.

“Binafsi, kama mkewe, nilipokea mapenzi yake kutaka achomwe kwa moyo mzito. Aliponiambia kuhusu uamuzi huo kabla yake kufariki, nilikataa. Hii ilimfanya asitoe maelezo zaidi baada ya kugundua kwamba sikukubaliana naye,” alisema Bi Amiana.

Aliendelea: “Tutanunua jeneza na kuweka majivu ndani na kulifunga. Kisha tutaweka picha yake juu ya jeneza watu waitazame kama vile wangekuwa wanatazama mwili wake.”

“Itakuwa sherehe ya kawaida ya mazishi ambayo tumezoea. Nilipokea mwili (majivu) katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta mnamo Januari 9,” aliongeza.

Marehemu aliyezaliwa Desemba 16 1939, alikuwa na wake wawili na watoto wanne.Mkewe wa kwanza, aliyetambuliwa kama Helena Etisi, alikuwa akiishi naye New Jersey, Amerika, huku Bi Amiana akiishi katika kijiji cha nyumbani.

Bi Amiana alisema watoto wote, pamoja na wale wake, wanaishi Amerika ambako walienda kuendeleza masomo yao.

Walihudhuria ibada ya kuchomwa kwa mwili wa baba yao na Bi Amiana alisema kwamba hawatahudhuria mazishi kijijini Kaunti ya Vihiga.

Bi Amiana alimtaja marehemu mumewe kama aliyekuwa mwenye upendo na msomi.

“Alipenda elimu na hakusahau jamii yake mashambani ya Elukongo,” alisema akiongeza kuwa kifo chake ni pigo kubwa.

Marehemu Etisi ndiye mwanzilishi wa kituo cha elimu ya chekechea cha Naomi ECDE, Emuhaya na mkewe alisema alianzisha taasisi hiyo kuweka msingi wa elimu wa watoto wakiwa wadogo.

  • Tags

You can share this post!

KINYUA KING’ORI: Ni haki ya kila Mkenya popote...

Fataki City wakialika Spurs EPL

T L