• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 8:50 AM
KINYUA KING’ORI: Vinara wa Azimio wana hoja nzito za kudondosha katika mikutano yao

KINYUA KING’ORI: Vinara wa Azimio wana hoja nzito za kudondosha katika mikutano yao

NA KINYUA KING’ORI

HATUA ya vinara wa Azimio la Umoja-One Kenya kuandaa mikutano ya hadhara maeneo mbalimbali nchini inasaidia kukumbusha serikali ya Kenya kwanza ahadi zao kwa raia.

Isitoshe, mikutano hiyo inadhihirishia serikali na Wakenya kwamba upinzani uko ngangari kutekeleza wajibu wake bila hofu.

Kila mara katika hotuba zake Rais William Ruto amekumbusha upinzani, hususan kinara Raila Odinga, kutekeleza kazi yao ya kutia presha serikali naye akitekeleza ya urais.

Upinzani unatimiza wajibu wake kusukuma serikali ibuni mbinu za kuimarisha uchumi na maisha ya mwananchi wa kawaida.Rais Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua wakome kumkejeli Bw Odinga anapozungumza na raia.

Wamakinike kuendesha vyema serikali hii, inayozidi kuumiza raia kwa ushuru ilhali gharama ya maisha inapanda kila uchao.

Upinzani una hoja nzito za kusukuma serikali izamie: kukwama kwa miradi ya maendeleo, kuboresha miundomsingi, kuimarisha kilimo ili taifa liwe na chakula cha kutosha, kueneza usambazaji maji safi na usafi, kuimarisha elimu bora na kukuza utoaji matibabu nafuu kwa raia wote.

Itakuwa hekima vinara wa upinzani wakidondosha mapungufu ya serikali tangu iingie mamlakani, badala ya kutoa matamshi ya uzushi au kushambulia maafisa wa idara huru katika mikutano yao.

Ni wazi kuwa fedha zinafujwa tangu Ruto awe rais, ufisadi unaendelea , ukabila unaongezeka katika kuajiri watumishi wa umma, watoto wengi maskini wamekosa elimu kwa ukosefu wa karo na pesa za mgao wa kaunti zimecheleweshwa hali ambayo inalemaza miradi ya maendeleo mashinani.

Je, nani atatia presha serikali ishughulikie masuala haya kwa dharura ikiwa si viongozi wa upinzani katika mikutano ya hadhara?

Hizo ndizo hoja Bw Odinga na vinara wenza wanafaa kuzishinikizia kabisa ili serikali ijue raia hawatokubali uchumi wa taifa na maisha yaendelee kuvurugika.

  • Tags

You can share this post!

Bungoma imegeuka mbingu yenye mungu, manabii na Yesu

NGUVU ZA HOJA: Lugha ya Kiswahili ina uwezo wa kuimarisha...

T L