• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
WARUI: Kufeli kwa wauguzi kunaibua maswali kuhusu mfumo wa elimu

WARUI: Kufeli kwa wauguzi kunaibua maswali kuhusu mfumo wa elimu

Na WANTO WARUI

ELIMU ya Kenya imejipata ikiwekwa katika mizani na kuzua maswali kadha baada ya wauguzi waliotarajiwa kwenda kufanya kazi Uingereza, kufeli maswali mboga ya Kiingereza.

Serikali ya Uingereza ilihitaji wauguzi mia tatu kuajiriwa nchini humo na serikali ya Kenya ilichukua juhudi za kuwezesha wauguzi hao kusafiri huko.

Kama ilivyo desturi, wauguzi hao walipewa maswali ya mahojiano kwa lugha ya Kiingereza kutoka vipengele mbalimbali ambavyo vina mtagusano wa kazi yao.

Ajabu ni kwamba wale walioweza kupita mtihani huo ambao ulikuwa mwepesi sana walikuwa ni 10 tu.

Wengine wote hawakuweza kuyajibu maswali mepesi ya Kiingereza.

Jambo hili limewaacha watu wengi wakijiuliza kama kweli elimu inayotolewa nchini imekamilika au ni ya mapito tu mradi mtu apate cheti.

Katika siku za nyuma, tumeshuhudia taarifa kuhusu wanafunzi waliowahi kuwa katika shule za upili ilhali hawajui kusoma.

Taarifa hizo zilisema kuwa kuna idadi kubwa ya wanafunzi ambao humaliza masomo bila kujua kusoma kabisa. Sasa mtu anaachwa akijiuliza ni vipi mtu akawa shuleni kwa zaidi ya miaka 10 na bado hajajua kusoma?

Je, hii ni kasoro ya walimu wetu au ni kasoro ya mfumo wa elimu unaotumika?

Hata hivyo, mtindo wa maisha wa Wakenya na mtazamo wao kuhusu elimu si mzuri kamwe! Asilimia 90 ya wananchi huambatanisha elimu na kuajiriwa hivyo basi kukosa kutambua umuhimu wake.

Wakenya wengi hujua kuwa elimu ni ya kumsaidia mtu apate kazi ya kuajiriwa tu.

Haya ni kinyume kabisa na matakwa ya elimu ambayo ni kumpa mtu maarifa ya kumwezesha kujiendeleza.Katika mataifa mengi hasa yale yaliyoendelea, watu husoma vitabu sana – wakiwa katika vyombo vya usafiri, mapumzikoni na nyumbani.

Hili huwafanya wapate maarifa zaidi ya kukabiliana na matatizo ya maisha. Kinyume na hayo, Wakenya huachana na vitabu punde tu wanapotoka masomoni.

Hata viongozi wetu hawashinikizi watu kusoma kwani hao wenyewe hawafanyi hivyo.

Uchaguzi mbaya wa mfumo wa elimu unaweza kuitia nchi na watu wake katika aibu kuu kama tulivyoona kutoka kwa wauguzi hawa waliposhindwa kujibu maswali ya Kiingereza.

Washikadau katika sekta ya elimu na viongozi wote kwa ujumla hawana budi kuhimiza wananchi kuelewa umuhimu wa kuendelea kusoma vitabu hata baada ya kumaliza masomo.

Ni vizuri kuondoa dhana iliyojaa vichwani mwa Wakenya wengi kuwa lengo la elimu ni kuajiriwa.

Wauguzi hao ambao wangepata mshahara wa takriban elfu mia nne kwa mwezi kila mmoja wangekuwa ni msaada mkubwa kwa familia zao na taifa.

  • Tags

You can share this post!

Nassir na Shahbal wabishania ‘Baba’

Kaunti 43 hazijatengea ‘Big 4 Agenda’, ripoti yasema

T L