• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
LEONARD ONYANGO: Serikali itoe chakula cha msaada kwa kaunti zote 47

LEONARD ONYANGO: Serikali itoe chakula cha msaada kwa kaunti zote 47

Na LEONARD ONYANGO

TAKWIMU za serikali zinaonyesha kuwa wakazi wa kaunti 23, hasa katika maeneo kame, wanahitaji chakula kwa dharura huku makali ya baa la njaa yakizidi kukeketa nchini.

Kulingana na ripoti iliyotolewa Jumatatu, wakazi wa kaunti nane; Garissa, Isiolo, Lamu, Mandera, Marsabit, Tana River, Turkana na Wajir wamelemewa zaidi na makali ya njaa na wanahitaji chakula cha msaada kwa haraka.

Wakazi wa kaunti nyingine 15 wanahitaji chakula cha msaada japo hawajalemewa sana ikilinganishwa na wenzao katika kaunti hizo nane.Kwa ujumla, serikali inasema kuwa Wakenya milioni 2.5 wanahangaishwa na njaa humu nchini na wanahitaji msaada.

Serikali inasema kwamba ilitumia Sh1.2 bilioni kununua chakula cha msaada kwa ajili ya waathiriwa wa njaa nchini kufikia mwezi jana.Serikali pia imetoa Sh450 milioni kwa wanajeshi wa KDF kununua mifugo waliodhoofika na chakula kwa ajili ya mifugo.

Wizara ya Maji pia imepewa Sh350 milioni kusambaza maji kwa Wakenya wanaokabiliwa na uhaba wa bidhaa hiyo uliosababishwa na ukame unaoendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Serikali inasema kwamba inalenga kutoa Sh5,000 kwa familia 369,000 na watu 734,119 walio hatarini zaidi kila baada ya miezi miwili kuwasaidia kukabiliana na njaa.Ni kweli kwamba kaunti 23 zinazolengwa na serikali zimelemewa na njaa kwa sababu maeneo hayo hukumbwa na uhaba wa mvua kila mwaka.

Mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha ukame wa muda mrefu yamefanya hali kuwa mbaya zaidi katika maeneo hayo.Vilevile, ni kweli kwamba kuna maelfu ya familia katika kaunti zilizosalia 24, ikiwemo Nairobi, wanaohitaji chakula cha msaada kwa dharura.

Makali ya janga la corona na ukame yamesababisha maelfu ya watu wanaoishi katika mitaa ya mabanda mijini kuishi kwa shida kutokana na ukosefu wa mahitaji muhimu.Mvua katika baadhi ya maeneo ya Nyanza, Bonde la Ufa, Pwani, Magharibi ilikuwa haba hivyo kuwaacha wengi wakihangaishwa kwa njaa.

Hivyo si sahihi kwa serikali kuchukulia kwamba kila mtu ameshiba katika kaunti 24 zilizosalia.Aidha, kiasi cha chakula ambacho kimekuwa kikitolewa kwa kila familia kinafaa kuwa kingi kuwatosha kutumia kwa angalau miezi minne.

Lakini kuwapa waathiriwa wa njaa ‘gorogoro’ moja au mbili ni sawa na mchezo wa ‘danganya toto’.Kifungu cha 43 (1)(c) cha Katiba kinasema kuwa kila Mkenya ana haki ya kushiba.

You can share this post!

FAUSTINE NGILA: Afrika isipojipigia debe Wikipedia...

TAHARIRI: Viongozi wasisute ovyo tume ya IEBC

T L