• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
WASONGA: Serikali ifute mikataba ghali ya ununuzi stima

WASONGA: Serikali ifute mikataba ghali ya ununuzi stima

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI inawavunja moyo Wakenya na wawekezaji kwa kutoa habari za kukanganya kuhusu suala muhimu la bei ya stima nchini, hali ambayo itaathiri mipango ya maendeleo nchini.

Mwezi mmoja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa bei ya kawi hii itapungua kuanzia mwezi wa Desemba mwaka huu, Wakili Mkuu wa Serikali Ken Ogeto alitoa taarifa inayokinzana na ahadi hiyo.

Rais Kenyatta aliunda kamati itakayosimamia utekelezaji wa mapendekezo ya jopokazi lililochunguza mikataba kati ya kampuni ya Usambazaji Kawi Nchini (KPLC) na kampuni za kibinafsi za uzalishaji kawi (IPPs).

Jopo kazi hilo lilipendekeza kuwa bei ya stima ipunguzwe kwa Sh16 kwa kipimo kimoja kutoka bei ya sasa ya Sh24; punguzo la asilimia 33.

Wajibu mkuu wa jopo kazi hilo ulikuwa ni kuchunguza uwezekano wa kuondolewa kwa mikataba ya ununuzi wa stima ambayo KPLC ilitia saini na kampuni hizo.

Hii ni baada ya kubainika kuwa chini ya mikataba hiyo IPPs zimekuwa zikiuzia KPLC kawi kwa bei ya juu kupita kiasi.

Hatimaye bei hiyo hupitishwa kwa wateja wa stima ambao ni Wakenya wa kawaida na wazalisha bidhaa.

Kwa hivyo, katika ripoti yao, wanachama wa jopo kazi hilo lililoongozwa na mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya usambazaji mafuta, Kenya Pipeline, John Ngumi, walipendekeza kuwa mikataba hiyo ya ununuzi wa stima ifutuliwe mbali.

Lakini mnamo Jumanne, Bw Ogeto aliwashangaza Wakenya alipowaambia wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Kawi kwamba KPLC haiwezi kufutilia mbali mikataba ya ununuzi wa stima kutoka kwa IPPs “kwani ni kinyume cha sheria.”

Wakili huyo Mkuu ambaye alimwakilisha Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki, alisema mikataba hiyo inaweza tu kafutiliwa mbali ikiwa kampuni hizo zitafeli kutekeleza wajibu wao kulingana na mikataba hiyo.

Hii ina maana kuwa Wakenya wataendelea kubebeshwa mzigo mzito wa gharama ya juu ya stima kutokana na mikataba kati ya KPLC na IPPs.

Kampuni hizo za kibinafsi ni; Rabai Power Ltd, Gulf Power Ltd, Thika Power Ltd, Triumph Power Ltd na Muhoroni Power Generating Plant.

Swali langu ni je, mbona KPLC ilitia saini mikataba ya ununuzi wa stima na kampuni hizi za kibinafsi ambazo huzalisha stima kwa kutumia mitambo inayotumia dizeli ilhali hununua stima kwa bei rahisi kutoka kampuni ya KenGen?

Mbona kampuni ya KenGen isiwezeshwe kuzalisha stima kupitia upepo, jua, au mvuke badala ya kutegemea pakubwa kawi inayozalishwa kwa maji ambayo hutegemea uwepo wa mvua?

Nahisi kuna sakata kubwa zaidi iliyopo katika mpango huu wa ununuzi wa stima kutoka kwa kampuni hizi zinazomilikiwa na watu binafsi.

Kwa mfano, akiongea Bungeni, kiongozi wa zamani wa wengi Aden Duale alifananisha mpango huo wa ununuzi wa stima kutoka IPPs kama “sakata kubwa kuliko Anglo Leasing.”

Mbunge huyo alikadiria kuwa mpango huo huwagharimu walipa ushuru karibu Sh400 bilioni kwa mwaka, kupitia bili za juu za stima.

Kimsingi, serikali inafaa kuipa KenGen uwezo wa kuzalisha umeme tosha ili iuzie KPLC badala ya kampuni hii kununua kawi hii kutoka kwa kampuni za kibinafsi, ambazo wameliki wao hawajulikani.

Kwa njia hii bei ya stima itapungua nchini na kwa manufaa ya raia na wawekezaji wa humu nchini na kutoka ng’ambo.

  • Tags

You can share this post!

Spurs wazidiwa ujanja katika gozi la Europa Conference...

MATHEKA: Kususia kura ni kuruhusu watu wabovu kutwaa uongozi

T L