• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
TAHARIRI: Serikali itoe ARVs bora kwa watoto ili kuzuia vifo

TAHARIRI: Serikali itoe ARVs bora kwa watoto ili kuzuia vifo

Na MHARIRI

KWAMBA Kenya imeorodheshwa kuwa nchi bora zaidi barani Afrika kuhusiana na uzuiaji wa maambukizi ya HIV kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni habari njema kweli.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi punde kutoka Baraza la Taifa la Kudhibiti Ukimwi(NACC), nchi imepunguza kiwango cha maambukizi ya HIV kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa hadi asilimia 10.

Lakini wataalamu wametahadharisha kuwa ni jambo lisilokubalika kuwa na visa vya maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto katika zama hizi, kutokana na maendeleo ya teknolojia ya matibabu.

Jambo linalotia wasiwasi zaidi ni kwamba kati ya watoto 106,807 walio na virusi vya Ukimwi wenye umri wa miaka 15 na chini nchini Kenya, ni 72,241 pekee wanaopata matibabu.

Watoto hawa wanapokua na kuwa watu wazima pana uwezekano wa vita dhidi ya Ukimwi kutatizika zaidi.

Cha kusikitisha zaidi ni kwamba, ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa wiki hii inaonyesha kuwa ARVs hazifanyi kazi kwa asilimia 10 ya watoto walio na virusi vya Ukimwi nchini Kenya.

Dawa hizo, ambazo ni pamoja na doravirine, etravirine na rilpivirine, zinatumika kote nchini.Ripoti hiyo inabainisha kuwa nchi nyingi zimeacha kutumia dawa hizi, ambazo pia hujulikana kama NRTIs, kwani haziwezi kukabiliana na virusi kwa watoto.

Huku serikali ikitangaza mipango ya kuziondoa dawa hizi ili kupendelea dawa aina ya dolutegravir ambayo ni bora zaidi kwa watoto, haijulikani ni lini dawa zinazofaa zaidi kwa watoto zitapatikana.

Serikali, kupitia Wizara ya Afya, inapaswa kuharakisha kuhakikisha kuwa dawa hizo nafuu kwa mtoto zinapatikana ili kuzuia vifo zaidi vya watoto.

Pia kuna haja ya kuzuia kabisa maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuhakikisha kuwa watoto wote walio na virusi hivyo wanatambuliwa na kupewa dawa.

Kampeni hii inapaswa kupanuliwa kwa vikundi vya rika zote ikiwa vita dhidi ya Ukimwi vitafanikishwa barabara humu nchini na kumlinda mtoto na mama yake.

Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duninani yatutie shime kuweka mikakati kabambe ya kuzuia vifo vya watoto wetu. Juhudi zahitajika kotekote, serikali, wazazi na jamii kwa jumla ili kuangamiza jinamizi hili linalotatiza jamii.

You can share this post!

KPA imeajiri Wapwani kupita kiasi, yadai ripoti

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Umuhimu wa kutoa zakah katika jamii...

T L