• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
TAHARIRI: Changamoto za CBC zilizobaki zitatuliwe

TAHARIRI: Changamoto za CBC zilizobaki zitatuliwe

NA MHARIRI

WANAFUNZI wa Gredi 7 hatimaye walienda shuleni jana Jumatatu baada ya pandashuka nyingi kuhusu hatima yao.

Safari ya elimu ya wanafunzi hao ambao ndio wa kwanza kutekeleza mtaala wa CBC imekuwa ndefu, na bado inakumbwa na changamoto.

Kuanzia katika maandalizi ya mitihani yao ya kitaifa waliofanya katika Gredi ya 6, hadi kupitia swintofahamu kuhusu kama wangejiunga na Gredi ya 7 katika Shule za Upili au za Msingi, imekuwa ni hali ya kuwakanganya pamoja na wazazi na walimu wao.

Katika safari hii mpya ambayo sasa inaendelezwa chini ya utawala mpya wa serikali, itakuwa muhimu kuchukulia changamoto zote za mwanzoni kama mafunzo ili kuziepusha kurudiwa tena hatua zinapoendelezwa mbele.

Utawala wa sasa ulianza vyema, kwa kuchukua hatua ya kukusanya maoni ya wadau kuhusu yale yanayofaa kufanywa.

Ni kupitia kwa hatua hiyo ambapo iliamuliwa kuwa, wanafunzi hao waendelee kuwa chini ya Shule za Msingi badala ya Upili ilivyokuwa imepangwa awali.

Kwa sasa, bado kuna changamoto nyingine kadha ambazo zinahitaji kutatuliwa haraka iwezekanavyo.

Miongoni mwao ni kuhusu kuwepo kwa walimu wa kutosha kufunza Sekondari Msingi kwa mfumo wa CBC.

Kumekuwa na malalamishi kwamba, hakuna idadi ya kutosha ya walimu waliopokea mafunzo kufunza katika madarasa hayo.

Hili ni suala zito ambalo lazima asasi husika za serikali zitilie maanani na litatuliwe kwa dharura.

Mbali na hayo, shule nyingi za msingi hazikuwa zimejiandaa kuendeleza madarasa hayo.

Hii ni kumaanisha kuwa, hapauwepo mipango ya kutosha ya kuweka rasilimali na miundomsingi ya kutosha mapema kabla shule zifunguliwe.

Ripoti kwamba serikali ishatafuta ufadhili wa kuboresha miundomsingi ya shule hizi ni za kutia moyo.

Tunatumai kwamba, mipango yote ya kujenga na kuboresha miundomsingi muhimu ya kuendeleza elimu ya sekondari msingi itatekelezwa kwa njia ya uwazi itakayoleta manufaa kwa wanafunzi.

Wizara ya Elimu na wadau wengine wa sekta hii wafahamu kuwa, sasa hakuna wakati wa kulala kuhusu utekelezaji wa CBC.

Hatungependa kuona hali ya kwamba hatua zitaanza kupigwa kuenda nyuma katika siku za usoni, na kuwaacha kwa mataa watoto ambao tayari washaanza elimu chini ya mfumo huu mpya.

Wazazi na walimu pia sasa waache uzushi kuhusu elimu hii. Wafikirie kuhusu hatima ya watoto ambao tayari wameanza mafunzo ya CBC, na badala ya kupinga watoe mapendekezo yao kuhusu jinsi ya kuboresha matatizo ambayo wanayaona.

  • Tags

You can share this post!

Napoli watandika AS Roma na kufungua pengo la alama 13...

Gaspo Women kutoana jasho na Kayole Starlets katika KWPL

T L