• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
TAHARIRI: Idara nyingine za serikali ziipe umuhimu lugha ya Kiswahili

TAHARIRI: Idara nyingine za serikali ziipe umuhimu lugha ya Kiswahili

NA MHARIRI

UZINDUZI wa Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa lugha ya Kiswahili ni hatua nzuri inayofaa kupongezwa.

Afisi ya Mkaguzi Mkuu, Bi Nancy Gathungu ilichapisha taarifa ya matumizi ya fedha za mwaka 2019/2020 kwa lugha ya Kiswahili.

Hii ni hatua nzuri katika kufikia matakwa ya Katiba, ambayo inatambua kuwa lugha mbili kuu za nchi ni Kiswahili na Kiingereza. Kiswahili ndiyo iliyowekwa mbele kwa kuwa ndiyo lugha inayozungumzwa na kueleweka na asilimia kubwa ya wananchi.

Hata wale ambao hawajawahi kwenda shule, wanaelewa kwa urahisi lugha hiyo iliyo na asili yake humu nchini, badala ya Kiingereza.

Katika kutaka kuonyesha usomi au kuwa na elimu, Wakenya wengi hujifanya kutoielewa lugha ya Kiswahili. Hujieleza kwa Kiingereza kuwa hawaifahamu lugha hiyo, ila ajabu ni kuwa, wanapokuwa katika shughuli zao za kibinafsi, hawawasiliani na jamaa na marafiki kwa Kiingereza.

Kuchapisha ripoti kuhusu jinsi pesa za umma zilivyotumika kutawawezesha wananchi wengi kufahamu na kufuatilia kwa karibu pesa zao zinavyotumika.

Aidha, ripoti hizo zitawapa raia uwezo wa kushiriki kikamilifu kwenye mikutano ya kuwashirikisha kuamua kuhusu miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Katiba inaeleza kuwa Kaunti ya Serikali ya Kitaifa haziwezi kuunda bajeti bila ya kuchukua maoni ya wananchi. Iwapo kwa mfano itagundulika kuwa pesa za mradi fulani hazikutumika vyema, wananchi wakielewa maelezo hayo kwa Kiswahili, watakuwa na uwezo wa kudadisi kwa kina.

Uchapishaji wa ripoti hiyo si jambo geni. Serikali hutumia Kiingereza na Kiswahili kwenye nyaraka zake, kama zile za maombi ya kuzaliwa au kupata vitambulisho.

Kilicho tofauti hapa ni umuhimu wa ripoti zenyewe kwa wananchi.

Mnamo Novemba 2020, Bunge la Kitaifa lilizindua Kanuni za Kudumu kwa lugha ya Kiswahili.

Kwa bahati mbaya, wabunge walilifanyia mzaha suala hilo, na mijadala yao wakati huo ilionyesha walijilazimisha tu, na kamwe si jambo wanaloamini kuwa lina umuhimu.

Sasa hivi, nyaraka ratiba za siku za bunge zinaendelea kuchapishwa kwa Kiingereza na ni wabunge wachache wanaozungumza kwa Kiswahili.

Si lazima kwa maafisa wa Afisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kuzungumza Kiswahili, lakini mchakato ulioanzishwa wastahili kuendelezwa. Kufanya hivyo, kutawapa sauti mamilioni ya Wakenya wanaoweza kusoma Kiswahili kwa wepesi.

You can share this post!

Ukimwi: Himizo watu waendelee kubaini hali zao

IEBC: 5,800 kuwania viti bila vyama

T L