• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
TAHARIRI: Itakuwa aibu raia mwenye njaa kuombwa kura

TAHARIRI: Itakuwa aibu raia mwenye njaa kuombwa kura

NA MHARIRI

MAELFU ya wananchi katika pembe tofauti za nchi wanatarajiwa kuendelea kukumbwa na makali ya njaa mwaka huu 2022.

Hii ni baada ya idara ya utabiri wa hali ya hewa kubainisha kuwa, kuna uwezekano mvua haitanyesha kwa kiwango cha kutosha katika baadhi ya maeneo ya nchi msimu huu.

Mwaka uliopita, 2021 kiangazi kilidumu kwa muda mrefu na kusababisha hasara tele ambapo maelfu ya mifugo waliangamia kwa kukosa lishe, huku binadamu wakitaabika kwa kukosa chakula na maji ya kutosha.

Inasikitisha kuwa, katika karne hii, nchi ya Kenya iliyoendelea kiteknolojia bado inasikika ikilalamikia ukosefu au uhaba wa mvua kuwa chanzo cha kushindwa kutosheleza mahitaji ya chakula kwa raia wake.

Serikali za kaunti ambazo zilitwikwa jukumu la kusimamia kilimo zimefeli kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo katika sekta hiyo.

Wakati huu wa kampeni, wanasiasa hawataona aibu kuzuru sehemu za nchi ambapo raia wanakumbwa na njaa ili kuomba kura, ilhali wakati wako mamlakani hawajitahidi kutekeleza suluhu za kudumu ambazo zitapunguza madhara haya ya kiangazi yanayoshuhudiwa kila mara.

Wakati mwingi unaposafiri nje ya nchi au kutangamana na raia wa kigeni humu nchini, hutakosa kusikia jinsi wanavyomiminia sifa Kenya kwa hatua zilizopigwa kukumbatia teknolojia za kisasa katika nyanja mbalimbali ikilinganishwa na nchi nyingine nyingi za Afrika.

Hakika, kuna aina nyingi za teknolojia ambazo pia zimeanzishwa katika sekta ya kilimo.

Hizi zinajumuisha mbinu za unyunyizaji maji mashambani, utoaji ushauri wa kilimo, utengenezaji wa mbegu za mimea mbalimbali zinazoweza kustahimili kiangazi, njia za kisasa za kuhifadhi mazao, miongoni mwa mengine.

Hata hivyo, mbinu hizo zote zimesalia kutumiwa sana na waekezaji wa kibinafsi wanaomiliki mashamba makubwa huku ikiwa vigumu kwa wakulima wadogo kuzitumia.

Inatakikana shinikizo itolewe kwa wadau wote wanaohusika na ustawishaji wa kilimo serikalini kutilia maanani hitaji la kuwezesha wakulima wadogo kukoma kutegemea mbinu za kilimo zilizopitwa na wakati.

Serikali za kaunti zijitenge na matumizi mabaya ya fedha na badala yake zijitahidi kuwekeza katika uzalishaji na uhifadhi wa lishe inayotosheleza mahitaji ya wananchi.

Pesa ambazo serikali ya kitaifa, za kaunti na mashirika mbalimbali huutmia kila mwaka kusambaza vyakula vya msaada zinaweza kusaidia kutekeleza suluhisho za kudumu ikiwa viongozi husika watajitolea.

You can share this post!

Blazers ina kibarua kigumu msimu huu

NTSA yatoa mafunzo mapya kwa madereva

T L