• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
TAHARIRI: Mauaji: kaunti zitenge bajeti za kukabili maradhi ya akili

TAHARIRI: Mauaji: kaunti zitenge bajeti za kukabili maradhi ya akili

NA MHARIRI

KATIKA siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la habari kuhusu visa ambapo watu wanaangamiza jamaa au watu wa karibu.

Ndani ya mwezi mmoja uliopita, zaidi ya visa 40 vya watu kuua jamaa, marafiki au majirani vimeripotiwa katika vyombo vya habari.

Bila shaka, kuna vingine vingi ambavyo havikuripotiwa.

Jana, pekee visa visivyopungua vitano vya mauaji ya aina hiyo viliripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mfano, mwanaume aliua mpenzi wake wa zamani kwa kumchinja kabla ya kuuawa na wakazi wenye ghadhabu katika Kaunti ya Murang’a, jana.

Katika eneo la Baringo ya Kati, maafisa wa polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na kisa ambapo mwanaume alikata mkono mkewe na kisha kujaribu kujitoa uhai.

Wakazi wa kijiji cha Murubara, Kaunti ya Kirinyaga, walipigwa na butwaa baada ya mwanaume kudaiwa kuua mkewe na kisha kuchoma mwili wake.

Katika kaunti hiyo, maafisa wa polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na kisa ambapo miili ya watu watatu; mume, mke na mtoto wao, ilipatikana katika eneo la Ndia.

Polisi wanaamini kuwa mwanaume aliua mke na mtoto wake na kisha kujitoa uhai.

Jambo ya kusikitisha ni kwamba huku visa vya mauaji ya aina hii vikiendelea kuongezeka, hakuna hatua zinazochukuliwa na serikali. Serikali za kaunti na kitaifa zimesalia kimya. Mauaji hayo yanaonekana kuwa jambo la kawaida.

Lakini ukweli ni kwamba mauaji hayo inaweza kuwa ishara ya hali mbaya ya afya ya akili nchini. Idadi kubwa ya Wakenya wamelemewa na msongo wa mawazo kutoka na sababu mbalimbali – ikiwemo hali ngumu ya uchumi.

Idadi ya waathiriwa wa magonjwa ya akili inaongezeka kila uchao lakini hawapati huduma za matibabu kutokana na gharama ya juu.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa asilimia kati ya asilimia 20 na 25 ya wagonjwa wanaoenda katika hospitali za humu nchini wanahangaishwa na maradhi ya akili. Inakadiriwa kuwa kwa kila Wakenya 10, mmoja anahangaishwa na maradhi ya akili.

Mnamo 2020, jopokazi la kuchunguza madhara ya magonjwa ya akili lililoongozwa na Profesa Frank Njenga lilipendekeza maradhi hayo kutangazwa kuwa janga la kitaifa kutokana na idadi kubwa ya waathiriwa.

Mnamo Juni 2022, Rais Uhuru Kenyatta – ambaye sasa ni mstaafu – alitia saini Sheria ya Afya ya Akili.

Sheria hiyo inalazimisha serikali za kaunti kutenga bajeti kwa ajili ya afya ya akili.

Serikali za kaunti hazina budi kuhakikisha kuwa wakazi wanapata huduma za afya ya akili bila malipo au gharama nafuu ili kupunguza visa vya watu kuangamizana kutokana na misongo ya akili.

You can share this post!

Wanasiasa wamwekea Ruto mtego, atakubali kunaswa na presha...

KDF kutumia mabilioni DRC Wakenya wakiendelea kuumia...

T L