• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
TAHARIRI: Mradi wa Talanta Hela usiwe maneno tu, utekelezwe

TAHARIRI: Mradi wa Talanta Hela usiwe maneno tu, utekelezwe

NA MHARIRI

MNAMO Jumatano waziri wa Michezo Ababu Namwamba aliweka wazi azma ya serikali ya Kenya Kwanza kuinua spoti mashinani kwa kuwinda na kukuza kipawa katika kaunti zote nchini, shuleni na mashirika yote nchini ambayo yanajihusisha na michezo.

Akizindua kamati ya Talanta Hela, Waziri alisema kwamba atashirikiana na mashirika yote ya spoti na sanaa nchini kusaka, kuteua, kukuza na kutafutia soko ili kuuza talanta hizo ili kuzigeuza kuwa fedha kama njia ya kuwapatia ajira vijana husika.

Maono ya serikali ni kuweka hela mfukono mwa chipukizi wa kati ya miaka 10 na 19 ambao watapelekwa kwenye Akademia ya Kitaifa ya Spoti jijini Nairobi ili kunoa makali ya vipaji vyao kabla ya kuwatafutia nafasi za kazi husika serikalini, kampuni na mashirika makubwa nchini.

Ushauri kwa kamati ya Talanta ni kuanza mradi huu mara moja kote nchini bila kukawia ili kufikia mpango wa serikali kuzindua ligi kaunti zote 47 mashinani kabla ya mwaka huu kufikia mwisho. Kwa kuwa serikali ilipendekeza kutanguliza kwa fani ya kandanda kabla ya zile zingine, basi wataalamu wa soka mashinani wanafaa kuanza kuhusisha ili kujitosa kwenye harakati hizi za kuwinda vipawa hizi.

Kwa kuwa serikali imejitolea kuwekeza fedha nyingi kwenye mradi huu, haifai watekeleza kuonekana kuzembea au kuwa kizingiti kwa ufanisi wake.

Ni wajibu wa maafisa walioteuliwa kuongoza kamati hii ya Talanta Hela wakiwepo Mwenyekiti wake mwanahabri wa spoti Carol Radull, na wasaidizi wake mtupaji gwiji wa mkuki kimataifa Julius Yego, wanasoka majagina Boniface Ambani na Sammy Shollei kati ya wengine kibwebwe na kuanza kazi kwa kujitolea.

Macho yote kwa sasa yako kwa serikali kufadhili na kusimamia mradi huu ili kuona ndoto ya barobaro wa Kenya ikigeuzwa kuwa ukweli pale watakapotambua pesa mifukoni yao. Kando na spoti serikali iwaendee vijana wenye mapenzi ya kipekee katika sanaa ya uigizaji, muziki na fasheni kati ya ubunifu mwingine.

Kenya imekabiliwa na janga la ukosefu wa nafasi za ajira mbali na gharama ya maisha kuwalemea asilimia kubwa ya wananchi. Kupitia mfumo huu mahsusi wa serikali ya Rais Ruto, vijana watakuwa na kila sababu ya kutabasamu kwa kuondolewa dhiki katika maisha yao ya sasa.

Bila shaka, mradi huu utakuwa suluhisho kwa matatizo mengi yanayowakumba Wakenya yakiwepo matumizi ya mihadarati, wizi, ujangili, mauaji na mzongo wa mawazo unaopelekea wengi kujitoa uhai.

  • Tags

You can share this post!

Pasta afariki akiwa kwa mfungo bila maji, chakula kama Yesu

DOUGLAS MUTUA: Wanasiasa wa Mlima Kenya watumie akili au...

T L