• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:26 PM
DOUGLAS MUTUA: Wanasiasa wa Mlima Kenya watumie akili au waangamizwe

DOUGLAS MUTUA: Wanasiasa wa Mlima Kenya watumie akili au waangamizwe

NA DOUGLAS MUTUA

UKIKUTANA na Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro, mkumbushe “wajinga ndio waliwao”.

Uko radhi kuielekeza nasaha hiyo ya wahenga kwa eneo zima la Mlima Kenya. Ni onyo kwa watu wanaoona ugumu kutumia akili, wakaishia kujuta.

Eneo hilo likitumia akili kama kofia litaishi kutazama taifa hili likiongozwa na watu wa maeneo mengine, wenyeji walo wawe kama mitambo ya kupiga kura tu.

Habari zinazoenea kwa kasi huko ni kwamba Bw Nyoro atakuwa mwaniaji urais baada ya Dkt William Ruto kustaafu.

Mwenyewe ametanua kifua na kukiri anautamani sana urais.

Ni mapema kwa wanasiasa hao kuanza kumtukuza na kumkweza Bw Nyoro kama mwanasiasa gwiji zaidi wa Mlima Kenya, sikwambii kuota akiwa rais.

Kimsingi inaaminika kwamba Dkt Ruto – kutokana na ukwasi wake wa mikakati ya kisiasa – atatawala kwa mihula miwili, hivyo anayeota kumrithi anatazama mwongo mzima!

Ni sawa kwa Bw Ndindi kuanza kujishashashasha, hasa akifuata nyayo za Dkt Ruto ambaye kwa miaka 10 alipokuwa Naibu Rais alifanya kampeni za kuwa rais.

Hata hivyo, mazingira ya wakati huo na sasa ni tofauti kabisa: mbali na kuwa Naibu Rais, Dkt Ruto alikuwa kigogo wa ngome yake ya Rift Valley. Hilo halikutiliwa shaka.

Ziada ni ile ahadi ya ‘yangu 10, na ya William (Ruto) 10’ iliyotolewa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alipokuwa uongozini ikanata nyoyoni mwa watu.

Hali ilivyo kwa Bw Nyoro ni kwamba eneo analotokea lina kigogo kwa jina Rigathi Gachagua, ambaye ni Naibu wa Rais.
Siasa zilivyo, anayemkaribia rais kwa mamlaka huchukuliwa keshatangulia chanoni, hivyo tangazo la Bw Nyoro kujaribu kujikweza ni kumchokoza Bw Gachagua.

Ijapokuwa Dkt Ruto hajaahidi hadharani kumrithisha Bw Gachagua urais, pia hajatoa ahadi hiyo kwa Bw Nyoro. Hatari ya kimsingi iliyopo ni kuwa wenyeji wa Mlima Kenya ambao wanamtambua Bw Gachagua kutokana na cheo chake watamchukulia Bw Nyoro kama mtoto mchokozi.

Mambo yatamwendea tenge Bw Nyoro ikiwa eneo hilo litashuku anatumiwa na ‘wageni’, yaani watu wasio na asili ya Mlima Kenya, kumdhalilisha Bw Gachagua.

Ni rahisi sana kwa uvumi wa aina hiyo kuenea na kuaminika kwa kuwa kila Mkenya anajua ni kawaida kwa naibu rais kuchokonolewa na watu, akiwemo rais mwenyewe!

Hiyo imekuwa historia yetu tangu tulipopata uhuru 1963; makamu (naibu) wa marais Jomo Kenyatta, Daniel Moi, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta walidhalilishwa ajabu.

Mkosi huo ukimkumba Bw Gachagua, na wafuasi wake waamini chanzo chake ni Rais Ruto, huo utakuwa mwanzo wa utengano wa kisiasa kati ya Dkt Ruto na eneo hilo!

Wanasiasa wote wa eneo hilo watakaofungamana na Rais Ruto, akiwemo Bw Nyoro na wanaompotosha kuanza kampeni mapema hivi, watageuka nyama ya nguruwe Saudia. Atakayenufaika kutokana na utengano huo ni Rais Ruto mwenyewe na Waziri Musalia Mudavadi. Ikiwa Dkt Ruto anataka kutalikiana na eneo la Mlima Kenya kisiasa ili awe huru kumkuza na hatimaye kumtawaza mrithi wake, fursa ndiyo hii.

Bw Mudavadi, asiyeficha nia yake ya kumrithi Dkt Ruto, atakuwa katika nafasi bora ya kutimiza ndoto yake hiyo kwa kumshinikiza Dkt Ruto amtawaze.

Kwa ujinga wa wanasiasa wa Mlima Kenya, Bw Mudavadi atakuwa ameshinda vita baridi vya uchu wa mamlaka ambavyo vimekuwa vikiendelea kati yake na Bw Gachagua.

Tangu hapo kazi ya kunguru kutafuta mlo huwa rahisi panzi wanapopigana; wakichoka anawaokota na kuwameza kwa raha zake.

Kazi kwa wanasiasa wa Mlima Kenya, wajanjaruke au waliwe kwa ujinga wao!

[email protected] 

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Mradi wa Talanta Hela usiwe maneno tu, utekelezwe

Wabunge wa ODM waogopa ‘cheo’ cha Raila

T L