• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
TAHARIRI: Mwelekeo wa soka utolewe kamati shikilizi ikiondoka Mei 11

TAHARIRI: Mwelekeo wa soka utolewe kamati shikilizi ikiondoka Mei 11

NA MHARIRI

MASWALI chungu nzima yanaendelea kuibuliwa kuhusu hatima ya soka ya Kenya huku Kamati Shikilizi iliyobuniwa na serikali kusimamia mpira huo nchini ikitarajiwa kuondoka mamlakani siku 11 zijazo.

Kamati hiyo iliundwa mnamo Novemba 11 mwaka jana baada ya uliokuwa uongozi wa FKF kuondolewa mamlakani na Waziri wa Michezo Balozi Amina Mohamed kutokana na ubadhirifu wa fedha.

Kufikia makataa ya Mei 11, kamati hiyo itakuwa imehudumu kwa muda wa miezi sita na ni dhahiri kuwa muda wao kuwa kwenye usukani hautarefushwa.

Kwa sasa, Jaji Mkuu Mstaafu Aaron Ringera ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo ya muda na wanachama wake, wamekuwa wakiendesha shughuli za kupokea maoni kutoka kwa washikadau mbalimbali kuhusu katiba mpya ya FKF.

Kati ya waliowasilisha maoni yao kuhusu katiba hiyo ni wakuu wa timu zinazoshiriki KPL, NSL, WPL, Ligi za Divisheni ya Pili na wakuu wa mashirikisho ya FKF ya kaunti mbalimbali.

Mwanzo, ni vyema kusema kuwa tangu kuondolewa kwa waliokuwa wakuu wa FKF wakiongozwa na Nick Mwendwa na Katibu Mkuu Barry Otieno, kuna mabadiliko machache ambayo yameshuhudiwa.

Wanahabari hawanyanyaswi wala kuzuiliwa kufuatilia mechi mbalimbali jinsi ambavyo ilikuwa wakati wa Mwendwa.

Vilevile, uongozi wa klabu umekuwa huru kuendesha shughuli zao kama kupeperusha mechi zao, jambo ambalo halikuruhusiwa wakati wa utawala uliopita.

Vilevile wachezaji wa Harambee Starlets ambao walikuwa kambini kujifua kwa mechi za Mataifa Bingwa Afrika (AWCON) dhidi ya Uganda mnamo Februari walilipwa marupurupu ya kuwa kambini na hata baadhi ya wachezaji kupokezwa ajira.

Wakati wa utawala wa FKF wachezaji walikosa marupurupu na waliothubutu kulalamika walitimuliwa kutoka kwa timu ya taifa kwa kuonekana kama adui wa FKF.

Ingawa wamefanya kazi vizuri, pandashuka zilizozingira kamati shikilizi ni kutowalipa marefa kwa wakati, kuchelewesha mgao walioahidi kwa klabu za soka na kutowachukulia hatua baadhi ya waamuzi wanaodaiwa wamekuwa wakishiriki upangaji matokeo ya mechi.

Mkutano wa kubandua rasmi NEC ya FKF ambao unaendeshwa na matawi ya soka nchini nao unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa Mei, wakati ambapo kamati shikilizi ya soka itakuwa ishaondoka mamlakani.

Licha ya uwepo marufuku ya Fifa, wengi wanahoji ni vipi mechi tano za ligi ambazo zitakuwa zimesalia wakati huo zitaendelea.

Kwa hivyo, Mohamed anafaa kutoa mwelekeo kuhusu suala hili.

You can share this post!

Vituko vilivyoshuhudiwa wakati wa ibada ya kumuaga Kibaki

Askofu Muheria ahimiza wanasiasa waige mfano wa Kibaki

T L