• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Askofu Muheria ahimiza wanasiasa waige mfano wa Kibaki

Askofu Muheria ahimiza wanasiasa waige mfano wa Kibaki

NA SAMMY WAWERU

ASKOFU wa Kanisa la Katoliki jimbo la Nyeri, Anthony Muheria amewataka wanasiasa waige mfano wa Rais mstaafu Mwai Kibaki anayezikwa nyumbani kwake eneo la Othaya leo Jumamosi, Aprili 30, 2022.

Muheria ametoa himizo hilo wakati akihubiri kabla ya kuzikwa kwa Mzee Kibaki, ambaye alihudumu kama Rais wa tatu wa Kenya kuanzia 2002 hadi 2013.

Rais Kibaki alifariki Ijumaa, Aprili 22, 2022 akiwa na umri wa miaka 90.

“Akiwa mamlakani na hata baada ya kustaafu hakurushia wakosoaji wake cheche za maneno. Alichofanya ni kuzua utani na alikuwa mwenye heshima,” akasema.

Rais Uhuru Kenyatta ameliongoza taifa katika hafla hiyo ya kumpa heshima za mwisho Mzee Kibaki, ambaye ametajwa kama Shujaa kutokana na miradi ya maendeleo aliyotekeleza, ikiwa ni pamoja na kuboresha uchumi.

Naibu wa Rais, William Ruto, kiongozi wa ODM, Raila Odinga ambaye alihudumu kama Waziri Mkuu chini ya serikali ya mseto iliyoongozwa na Rais Kibaki, mawaziri, magavana, wanasiasa na viongozi wengine mashuhuri ndani na nje ya nchi pia wamehudhuria mazishi hayo.

Kwenye mahubiri ya Askofu Muheria, hakusita kutoa wosia kwa wanasiasa hasa Kenya inapojiandaa kushiriki uchaguzi mkuu mwaka huu.

“Tusafishe midomo na mikono yetu. Mzee Kibaki alipenda nchi hii na kila alipozungumza alielezea alivyoipenda. Tusiharibu picha ya msingi huo,” Askofu akahimiza, akiwataka wanasiasa kuwa makini haswa wanapoendeleza kampeni.

Malumbano ya kisiasa yanaendelea kushuhudiwa, mirengo inayomuunga mkono Dkt Ruto na Bw Odinga ikirushiana cheche za maneno hadharani.

Viongozi hao wametangaza nia yao kuwania urais Agosti 2022, wakionekana kuwa na uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wapigakura wakilinganishwa na wagombea wengine.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Mwelekeo wa soka utolewe kamati shikilizi...

Mpishi aliyekula akashindwa kulipa bili ‘April...

T L