• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:55 AM
TAHARIRI: Polisi waangalie upya mishahara ya maafisa wao

TAHARIRI: Polisi waangalie upya mishahara ya maafisa wao

KITENGO cha UHARIRI

IDARA ya polisi ni kikosi ambacho hutarajiwa kuwa na nidhamu. Maafisa wa polisi, sawa na wanajeshi na wengine wa usalama, hutarajiwa kutii maagizo bila ya maswali.

Katika utekelezaji wa majukumu yao, maafisa wa usalama ni watu wa kuitikia ‘Ndio bwana’ na kufanya kama wanavyoelekezwa. Kwa hivyo, mara nyingi huwa wanashughulikia kazi zao bila mapendeleo wala kushawishiwa na watu wengine, mbali na maagizo ya wakubwa wao.

Katika utekelezaji huu wa kanuni za kutii amri bila swali, sheria inawakataza maafisa wa usalama kujiunga na vyama vya kutetea wafanyikazi au kugoma. Ndio sababu maafisa wetu wa polisi wamekuwa wakiishi katika mazingira duni, wengi wakikosa nyumba nzuri, lakini hawajakuwa wakilalama hadharani.

Serikali kwa kuchukulia utii huo wa polisi, imechukua hatua ambayo huenda ikasababisha mtafaruku na kuhatarisha usalama wa nchi.Polisi ni wanadamu wenye hisia na wanaotegemewa na familia zao. Wakati huu ambapo wengi wanaishi nje ya kambi za polisi, ni makosa kwa Tume ya Huduma za Polisi (NPSC) kuwashusha vyeo maafisa ghafla bila ilani.

Maafisa wengi wa polisi waliokuwa wamepandishwa vyeo na kuwa mainspekta kutokana na kuwa na digrii, wamepigwa na butwaa kwa kugundua mshahara wao wa Novemba umekatwa. Inasemekana Idara ya Huduma za Polisi (NPS) iliamua kuwashusha kutoka kwa cheo ambacho mshahara ni Sh59,000 kwa mwezi hadi kile cha Sh32,000.

Baadhi ya maafisa hao walikuwa na mikopo ambayo walijua hata ilikatwa kwenye mishahara, walikuwa wakibaki na pesa za kulipa kodi, karo ya shule ya watoto wao na kadhalika.Lakini hatua ya kuwashusha vyeo ghafla ilisababisha wengine kupata hadi Sh18 pekee kwenye akaunti.

Mbali na kuwa hatua hiyo ni kinyume na kifungu cha 19 cha Sheria za Leba, kote ulimwenguni, hata nchi inapokuwa katika hali mbaya kiuchumi, mishahara ya maafisa wa usalama huwa haiguswi.Kufanya hivi hasa wakati nchi inapokumbwa na tishio la ugaidi, ni hatari kwa usalama wa raia.

Afisa aliye na digrii na bunduki bila kitu mfukoni ni hatari. Bila shaka atakuwa mfisadi. Hakuna kitakachowazuia maafisa wanaodaiwa kodi, kusimama barabarani usiku na kuweka misako ya kukusanya pesa. Kuna wengine wanaoweza kukodisha silaha zao kwa majambazi wavamie benki na maeneo mengine ya biashara ili wapate mgao.

Ikumbukwe tunaelekea wakati wa kampeni za uchaguzi ambapo wanasiasa wanaweza kuwakodisha maafisa wa usalama kuwa sehemu ya magenge yao. Hata polisi wasipoenda kortini, hatua ya serikali ni hatari, inayostahili kuangaliwa upya.

You can share this post!

Wasomali 4 wanaswa UG

Magavana mbioni kukamilisha miradi kabla ya kustaafu

T L