• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
TAHARIRI: Sekta ya afya hakika sharti irekebishwe

TAHARIRI: Sekta ya afya hakika sharti irekebishwe

NA MHARIRI

NI habari za kusikitisha kuwa maelfu ya miili ya watoto waliofariki katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) haijachukuliwa na wenyewe ili kuenda kuizika.

Kuna sababu mbili kuu za kutokea kwa hali kama hii; ama wenyewe wameshindwa kulipa bili ya hospitali ndipo waruhusiwe kuchukua miili hiyo, au jamaa wa watoto hao hawakuwepo watoto hao walipokufa, wakawatafuta na kukosa kuwapata.

Sababu kuu kati ya hizi mbili ni kushindwa kulipa bili ya hospitali, na kama desturi, hospitali kukatalia miili hiyo hadi madeni hayo yalipwe.

Hili ni tatizo ambalo limewasumbua Wakenya wengi kwa muda mrefu kiasi cha baadhi yao kuamua kuziachia hospitali miili ili ziizike.

Kipo kisa kimoja, na yakini vipo vingine vingi, ambapo bwana mmoja aliyefiwa na jamaa wake, aliiambia hospitali ‘chukueni (mwili) mkauzike basi’.

Kauli hii yenye mihemko ilikuwa baada ya mtu huyo aliyefiwa kudaiwa deni kubwa la bili ambalo hangeweza kulimudu. Kwa hasira akaiambia hospitali hiyo ipate hasara mbili, ipoteze pesa na kubeba gharama ya maziko.

Sharti visa kama hivi vimalizwe humu nchini. Matukio ya kuchangisha pesa za bili ya hospitali ni mengi sana nchini humu; hilo likiashiria kuwa Wakenya wengi hawawezi kumudu gharama ya matibabu.

Wengine kwa kushindwa na gharama, hukaa na wagonjwa wao majumbani hadi wanapojifia au wapone kwa neema ya Mola. Serikali yaweza kufanya nini ili kudhibiti hali hii? Sharti hospitali zote (za kibinafsi na za umma), yaani mfumo mzima wa afya, uwekewe mipaka ya bili.

Sharti kila ugonjwa uwekewe kiwango ambacho familia nyingi zinaweza kumudu. Hii ni kwa sababu hospitali zetu zina mazoea ya kutumia matatizo ya Wakenya kujinufaisha kupita kiasi.

Baadhi ya magonjwa yanayotibiwa kwa mamilioni ya pesa, nchini India ambako Wakenya wengi hukimbilia kwa matibabu hutoza chini ya robo milioni, kwa mfano.

Kufungamana na hilo, itakuwa muhimu pia serikali ya Rais William Ruto kuhakikisha kuwa kila Mkenya anapata kadi ya bima ya afya (NHIF) na kuwezeshwa kumudu ada ya kila mwezi ili Wakenya wote waweze kupata huduma za afya bila wasiwasi.

Hili linawezekana iwapo serikali itahakikisha kuwa sheria na sera mpya za afya zimetungwa.

Katika kutunga huko, mwananchi wa kawaida hasa yule mwenye pato la chini sana, azingatiwe. Yaani awe ndiye kama mhimili wa mchakato mzima wa kubuni sheria na sera mpya.

Ni muhimu zaidi pengo katika sheria ya sasa linalovipa vituo vya afya mwanya wa ‘kuminya’ Wakenya pesa liondolewe.Inapozingatiwa kuwa manifesto ya Rais Ruto ilitilia mkazo suala la afya, sharti tuanze kuona kwa vitendo hatua ikichukuliwa upesi.

You can share this post!

Murathe ahojiwa EACC kuhusu sakata ya ardhi mtaani Mukuru

Aliyekuwa kamishna wa ardhi ashtakiwa kwa njama ya kuuza...

T L