• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 9:49 AM
Aliyekuwa kamishna wa ardhi ashtakiwa kwa njama ya kuuza ardhi ya Sh30 milioni

Aliyekuwa kamishna wa ardhi ashtakiwa kwa njama ya kuuza ardhi ya Sh30 milioni

NA BRIAN OCHARO

ALIYEKUWA kamishna wa ardhi, Bw Wilson Gachanja, ameshtakiwa kwa madai ya kuhusika katika njama ya kuuza ardhi ya umma kwa kampuni ya kibinafsi katika Kaunti ya Kwale.

Katika kesi iliyoanza Jumatano, mahakama kuu ya Mombasa ilielezwa kuwa, ardhi hiyo inayodaiwa kuuzwa ina thamani ya Sh30 milioni.

Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkuu wa mahakama ya Mombasa, Afisa mkuu wa kushughulikia usajili wa ardhi, Bw Gordon Ochieng, alieleza kuwa ardhi hiyo ilikuwa imepeanwa kwa mwanasiasa wa Kwale Bw Boy Juma Boy mnamo Juni 23, 1994, ambaye alikuwa ametuma maombi ya kuimiliki.

Bw Ochieng alieleza kuwa, licha ya maombi ya kumiliki ardhi hiyo kukubaliwa, ununuzi wa ardhi hiyo ulifanyika kinyume cha sheria.

Ardhi hiyo kulingana naye, ilikuwa imetengwa kwa ujenzi wa barabara.

“Mchakato wa Bw Boy kumiliki ardhi hiyo na baadaye kuhamishiwa kwa kampuni ya M/S Galerius, ulifanyika kinyume cha sheria kwani ardhi hiyo ilikuwa imetengewa ujenzi wa barabara,” alisema shahidi huyo.

Bw Ochieng alieleza kuwa, uhamishaji usio halali wa ardhi hiyo, uligunduliwa na Tume ya maadili na kupambana na ufisadi(EACC).

EACC ilitaka kufahamu hatua zilizochukuliwa na Bw Gachanja kurejesha ardhi hiyo.

Katika kesi hiyo, Bw Gachanja, Bw Zablon Mabeya na Jabu Salim Mohamed, afisa wa zamani wa kusimamia mipango katika wizara ya ardhi, wote wanashtakiwa na kosa la matumizi mabaya ya afisi zao. Wameshtakiwa pia kwa kufumbia jicho unyakuzi wa ardhi hiyo.

Bw Mohammed anadaiwa kuandaa mpango wa ujenzi ambao si wa kweli na kuenda kinyume na haki za serikali ya kaunti ya Kwale.

Bw Gachanja na Bw Mabeya wameshtakiwa kwa kosa la kuandaa cheti kwa kupendelea kampuni ya M/S Galerius imiliki ardhi hiyo.

Mahakama ilielezwa kuwa, malalamishi ya ardhi hiyo kunyakuliwa yaliwasilishwa mara ya kwanza mnamo 1995, baada ya umma kuandamana kwa kuzuiwa kufika kwenye ufuo.

“Bw Gachanja alimfahamisha mwenye kampuni kuwa mchakato wa kumiliki ardhi hiyo ulikuwa umefutiliwa mbali, akimtaka kuwasilisha stakabadhi za umiliki ili zifutiliwe mbali,” alisema shahidi.

Kulingana na shahidi huyo, hatua ya Ms Galerius kutenga sehemu ili wananchi wapate njia ya kufikia ufuo ilikataliwa.

Kulingana naye, serikali ilitaka ardhi hiyo irudishwe yote licha ya kuwa ilikuwa imegawanywa.Kesi hiyo inaendelea kusikizwa.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Sekta ya afya hakika sharti irekebishwe

CECIL ODONGO: Teuzi za Rais Ruto za Makatibu wa Wizara...

T L